VIDEO: Bunge la Tanzania laridhia kutofanya kazi na CAG

Muktasari:

Bunge limeridhia kutofanya kazi na CAG, Profesa Mussa Assad baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kutoa kauli ya kulidharau Bunge kwa sababu alitamka kuwa chombo hicho ni dhaifu.


Dodoma:_Bunge limepitisha azimio la kutofanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad.

Uamuzi huo umepitishwa leo Jumanne Aprili 2, 2019 baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Haki,  Maadili na Madaraka ya Bunge,  Emmanuel Mwakasaka kuwasilisha na kusoma bungeni taarifa ya kamati hiyo iliyomhoji CAG,  kumtia hatiani baada ya kubaini kauli aliyoitoa kuwa Bunge ni dhaifu,  amelidhalilisha Bunge.

Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alitoa nafasi kwa wabunge kujadili jambo hilo huku wabunge wakipishana maoni yao,   kukubaliana na uamuzi huo na wengine kupinga akiwemo Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe.

Baada ya wabunge kutoa maoni yao,  Dk Tulia amelihoji Bunge kuhusu hoja hiyo, akiwakata wanaokubaliana na jambo hilo kusema ndio na wasiokubaliana na suala hilo kusema sio,  "waliosema ndio wameshinda. "

Wabunge wakimsikiliza Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kinga, Haki, Maadili, Madaraka ya Bunge, Emmanuel Mwakasaka alipokuwa akiwasilisha bungeni taarifa ya kamati yake kuhusu shauri dhidi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Profesa Mussa Assad la kulidharirisha Bunge, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Wabunge wakisoma kitabu cha taarifa ya Kamati ya Bunge ya Kinga, Haki, Maadili, Madaraka ya Bunge kuhusu shauri dhidi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Profesa Mussa Assad la kulidharirisha Bunge, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi