Bunge la Tanzania lashauri kadi ya NHIF kulipia kipimo cha MRI

Muktasari:

Bunge la Tanzania limeutaka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kushughulikia malalamiko ya wananchi kuhusu vifurushi vipya vya bima hiyo, likitaka iwe na uwezo wa kulipia gharama za kipimo cha MRI.

 


Dar es Salaam. Bunge la Tanzania limeutaka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kushughulikia malalamiko ya wananchi kuhusu vifurushi vipya vya bima hiyo, likitaka iwe na uwezo wa kulipia gharama za kipimo cha MRI.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi, Novemba 28, 2019 na mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, Peter Serukamba wakati wa uzinduzi wa vifurushi vya bima za afya ya NHIF katika uwanja wa Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Serukamba amesema kuna mengi yanayolalamikiwa na wananchi kuhusu huduma, kwamba ni muhimu kuyatatua.

“Kuna baadhi ya magonjwa yanapaswa kuangaliwa  na hata vipimo si wote wanaopima CT SCAN au MRI, vipimo hivi wanapima wachache, nadhani NHIF mlifikirie hili mtoe hii huduma katika kila kifurushi,” amesema Serukamba.

Akijibu hoja hiyo, mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi NHIF, Anne Makinda amesema suala la vipimo linafanyiwa kazi na baadhi ya mapendekezo yanaendelea kupokelewa.

 “Hili la vipimo tutalifanyia kazi, lakini pia watoa huduma msiwapime watu mara nyingi kipimo hicho kwa sababu ni mionzi, si vizuri msifanye hivyo ili kutengeneza fedha. Mtu apimwe kipimo hiki kwa utaratibu na pale daktari anapoona kuna ulazima wa kufanya hivyo,” amesema Makinda.

Makinda aliyewahi kuwa Spika wa Bunge la Tanzania kati ya mwaka 2010 hadi 2015 ametoa rai kwa hospitali na vituo vya afya kuhakikisha vinaboresha mazingira ya vituo ili kuwavutia wananchi wanaofika kupata huduma.

Amevitaka vituo vya afya vya umma na binafsi kutoa huduma nzuri kwa wagonjwa wenye bima.