CAG aagiza wajumbe wa kamati ya shule kuchukuliwa hatua

Dodoma. Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere ameshauri wajumbe wa kamati ya Ujenzi ya Shule ya Sekondari ya Kibaigwa iliyopo Kongwa kuchukuliwa hatua  baada ya kugundua madudu kwenye ujenzi huo.
Katika ukaguzi wake maalum alioufanya kwenye shule hiyo mwaka wa fedha 2018/2019, Kichere amesema mchakato mzima wa manunuzi haukuzingatia Sheria ya Manunuzi ya Umma wakati wa ukaguzi wa mchakato wa zabuni ya kumpata mkandarasi wa ujenzi huo.
Amesema alibaini kuwa mchakato wote wa manunuzi ulikuwa kinyume na Sheria ya Manunuzi ya Umma namba 21 ya Mwaka 2004.
Ameshauri wajumbe wa kamati ya ujenzi wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria hiyo kwa maofisa kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) waliohusika moja kwa moja na mradi ikiwa ni pamoja na kutoa maelekezo kwa uongozi wa Shule ya Sekondari Kibaigwa.
“Pia nilibaini kuwa, menejimenti ya shule ilipokea mabati 260 kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzana (TEA) kwa ajili ya kuezeka mabweni mawili. Matumizi ya mabati hayo hayakuweza kuletwa kwangu, hivyo nilishindwa kuthibitisha matumizi yake,”ameeleza kwenye ripoti hiyo.
Ametoa wito hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wafanyakazi waliohusika ikiwa ni pamoja na aliyekuwa mkuu wa shule hiyo kwa kipindi hicho na aliyepokea mabati hayo kama ilivyoainishwa kwenye taarifa.
Amesema walibaini hasara iliyotokana na ujenzi wa mabweni ya Sh 86.53milioni.
Amesema alipitia Ripoti ya Mthaminishaji Mkuu wa Serikali ya Aprili 2019 na kubaini thamani ya mabweni mawili ilikuwa Sh 60.58milioni.
Hata hivyo, amesema jumla ya malipo yaliyofanywa kwa mkandarasi wa ujenzi wa mabweni hayo ni Sh 147.12milioni ikimaanisha kuwa Serikali ilipata hasara ya Sh 86.53milioni.
“Ninashauri hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya mkandarasi aliyetajwa kwenye taarifa kwa kukiuka matakwa ya mkataba."