CAG abaini matumizi ya Sh2 bilioni Wizara ya Maliasili na Utalii kinyume na utaratibu

Muktasari:

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Tanzania (CAG) amebaini matumizi ya Sh2.58 bilioni yaliyofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii nje ya bajeti na kabla ya kupitishwa na Bunge.

Dar es Salaam. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Tanzania (CAG) amebaini matumizi ya Sh2.58 bilioni yaliyofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii nje ya bajeti na kabla ya kupitishwa na Bunge.

Hayo yamebainishwa katika ripoti kuu ya mwaka kuhusu ukaguzi wa taarifa za fedha za Serikali kuu kwa mwaka unaoishia Juni 30, 2019.

Fedha hizo zimetumika kufanikisha kampeni ya Urithi Festival Celebration and Channel maalum ya kutangaza vivutio vya utalii kinyume na taratibu.

“Nilipitia matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii na kubaini kiasi cha Sh2.58 bilioni kimetumika kuanzisha chaneli ya Televisioni “Urithi Festival” ili kutangaza vivutio vya utalii,” imeeleza ripoti hiyo.

Imeeleza kuwa katika kutambua chanzo ya kugharamia matumizi hayo,  hayakuwa na kifungu cha bajeti kama ilivyopitishwa na Bunge.

Imeeleza kuwa fedha hizo zilitolewa katika vifungu vingine vya matumizi ya wizara na taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo ambazo ni Tanapa, NCAA, Tawa na TFSA.

“Nilijulishwa kuwa bajeti ya Urithi Festival ilipitishwa na menejimenti ya Wizara katika vikao mbalimbali vilivyofanyika,” inaeleza taarifa hiyo.