CAG abaini udanganyifu wa mabilioni UDART, NEC na Wizara ya Maliasili na Utalii

Dodoma/Dar. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), amebaini udanganyifu wa mabilioni ya fedha kwenye maeneo matatu ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na taasisi za Serikali.

Hayo yamo katika ripoti ya ukaguzi wake iliyowasilishwa bungeni juzi, kuhusu hesabu za kipindi cha mwaka kilichoishia Juni 30, 2019.

Katika ripoti hiyo anataja maeneo aliyogundua udanganyifu ni pamoja na mradi wa mabasi ya mwendokasi (Udart), unaotekelezwa jijini Dar es Salaam, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Wizara ya Maliasili na Utalii.

CAG amebaini matatizo katika masuala ya mikataba ya uendeshaji wa miradi husika, kukiukwa kwa taratibu za zabuni na matumizi yaliyo kinyume na miongozo ya usimamizi wa fedha.

Mradi wa Udart

Kuhusu mradi wa mabasi ya mwendokasi unaotekelezwa kwa ubia na shirika la UDA na kampuni ya DART alibaini matatizo kadhaa, ukiwamo udanganyifu wa kuongeza bei ya ununuzi wa mabasi mapya 70 kinyume na mkataba wa ununuzi.

CAG alibaini mabasi hayo 70 yalinunuliwa kwa Dola 17.68 milioni (Sh40.5 bilioni) kwa mkataba ulioingiwa Septemba 30, 2017.

Hata hivyo, CAG alibaini mabasi hayo yalihamishiwa kwenye Kampuni ya Udart na Kampuni ya Simon Group kwa bei ya Dola 20.33 milioni (Sh47 bilioni) ikimaanisha kuwa kampuni hiyo ilipata faida ya Dola2.65 milioni (Sh6.1 bilioni).

Alisema pia makampuni ya Simon Group na Udart hayakuwasilisha taarifa katika Mfumo wa Forodha (Tancis) wa Mamlaka ya Mapato (TRA) juu ya uingizaji wa mabasi hayo.

“Matokeo yake mabasi yanashikiliwa na Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa zaidi ya siku 721 (Februari 2018 hadi Februari 2020) na yana deni la Dola2.3 milioni (Sh5.3 bilioni) kama gharama za utunzaji katika maghala ya mamlaka ya mapato,” alisema.

Kichere alisema pia uchunguzi ulibaini ununuzi mwingine wa mabasi 140 kwa kiasi cha dola 14.41 milioni (Sh33.3 bilioni) ambazo ni juu ya bei ya mkataba. Hata hivyo, mabasi yaliyowasili ni 138 tu.

Alisema mkataba wa mauzo ulionyesha muuzaji atatoa vipuri bure vya mabasi 84 yenye thamani ya Dola 13.37 milioni (Sh30.7 bilioni).

“Nilibaini kuwa vipuri vyenye thamani ya Dola 99,467 (Sh229.4 milioni) pekee ndivyo vilitolewa kwa Udart huku vilivyobaki vyenye thamani ya dola za Marekani 167, 958 (Sh387 milioni) vikiwa bado havijatolewa na wakala,” alisema.

Alisema kampuni ya Simon Motors haijakabidhi vipuri vilivyosalia, hivyo akaitaka Udart iombe kurejeshewa nyongeza ya bei ya manunuzi ya mabasi 138 au ikabidhiwe mabasi 70 yaliyohamishwa na Kampuni ya Simon Group Limited bila ya malipo.

CAG, alisema ukaguzi wake pia ulibaini udanganyifu wa malipo ya hisa ya zaidi ya Sh500 milioni kwa Mamlaka ya Soko la Hisa na Mitaji (CMSA) ambayo imekana kupokea fedha hizo.

Kuhusu mifumo ya Tehama uchunguzi wake umebaini Udart iliipa kampuni ya Maxcom Africa jumla ya Sh3.91 bilioni, bila kuwapo mkataba.

Alisema pia alibaini malipo ya Sh3.45 bilioni kwenda kwenye akaunti binafsi ikielezwa kuwa fedha hizo zitatumika kulipia fidia na hisa kwa wamiliki wa daladala.

Kichere aliishauri menejimenti ya Udart ichukue hatua za kisheria dhidi ya Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni hiyo pamoja na mhasibu wa UDA kwa udanganyifu uliopelekea ubadhirifu wa fedha.

Alisema kampuni ya Simon Media Group ilipewa mkataba wa kufanya usafi kwenye mabasi na vituo vya mabasi ya mwendokasi kwa kipindi cha kuanzia Mei 6, 2016 hadi Aprili 29, 2017.

Hata hivyo, ukaguzi wa CAG ulibaini kuwa kampuni iliendelea kutoa huduma licha ya mkataba wake kumalizika na ililipwa Sh698.54 milioni hadi kufikia Januari 2020.

Pia, CAG alibaini kuwa kuanzia Novemba 22, 2016 hadi Mei 3, 2018, kampuni ya Udart iliilipa Simon Media Group jumla ya Sh1.01 bilioni kama ujira wa matangazo, wakati hakukuwa na mkataba juu huduma hiyo.

Tume ya Uchaguzi

CAG pia ameeleza jinsi NEC ilivyokiuka taratibu za ununuzi na kutumia zaidi ya Sh6.3 bilioni kununua mahema yasiyo na ubora.

Hayo yamejitokeza wakati NEC ikiwa imekamilisha awamu ya kwanza ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kuandikisha zaidi ya wapiga kura milioni 30.

Ripoti hiyo inayoeleza hesabu za Serikali kuu hadi kufikia Juni 30, 2019, imetaja mapungufu ya mkataba kati ya NEC na kampuni ya Mzabuni aitwaye Yell Ltd ulioingiwa Aprili 11, 2019.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, NEC iliingia mkataba na mzabuni huyo kwa ajili ya ununuzi wa mahema 2,237 yenye thamani ya zaidi ya Sh6.3 bilioni na ulitakiwa kutekelezwa ndani ya siku 60 kwa ajili ya maboresho ya daftari la kudumu la wapiga kura.

“Ukaguzi ulibaini kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi haikufanya tathimini ya kina ili kuweza kubaini uwezo wa kifedha wa mzabuni, utaalamu pamoja na vifaa kinyume na kifungu cha 53 cha sheria ya ununuzi wa umma ya mwaka 2011 (kama ilivyorekebishwa mwaka 2016),” imesema ripoti hiyo, hatua iliyosababisha mzabuni kuwasilisha mahema yasiyokuwa na ubora.

Pia CAG alisema NEC haikumshirikisha mwanasheria mkuu wa Serikali katika mkataba.

Kama hiyo haitoshi, CAG amebainisha kucheleweshwa malipo ya awali kwa mzabuni hali iliyosababisha mzabuni mahema kupatikana nje ya siku 60 za mkataba.

Wizara ya Maliasili na Utalii