CAG afafanua fedha kutofika elimu bila malipo

Dar es Salaam. Kusuasua kwa utoaji fedha za utekelezaji wa elimu bila malipo kunachangia kukosekana kwa miundombinu ya elimu katika shule za msingi na sekondari hali inayozorotesha utoaji wa elimu bora nchini.

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2018/19 imeeleza kuwa elimu bora inahitaji mazingira wezeshi yakiwamo miundombinu ya kutosha kama vyumba vya madarasa, maabara, vyoo, mabweni, madawati na nyumba za wafanyakazi.

CAG Kichere anasema mwongozo wa utekelezaji wa elimu bila malipo uliotolewa Desemba 28, 2015 unaoelekeza ruzuku ya matumizi kwa kiwango cha Sh6,000 kwa kila mwanafunzi wa shule za msingi na Sh25,000 kwa mwanafunzi shule za sekondari hauko sawasawa.

Alisema tathmini aliyofanya kuhusu utekelezaji huo kwa mwaka wa fedha 2018/19 katika halmashauri 42 alibaini kulikuwa na upungufu wa Sh2.9 bilioni za matumizi zilizotumwa kwa shule za msingi na sekondari, sawa na asilimia 24 ya kiasi kilichotakiwa Sh12.29 bilioni.

Alisema kutopeleka fedha zilizopangwa kunazifanya shule kushindwa kununua vifaa muhimu vya elimu kama vitabu, zana za kufundishia, vifaa vya maabara na kemikali wala kufanya marekebisho madogomadogo ya miundombinu ya shule, kujenga uwezo, utawala, vifaa vya ofisi na gharama ya chakula.

“Kwa hiyo, sera ya Serikali ya kuboresha elimu nchini inaweza isitekelezwe kama ilivyopangwa. Ninaishauri Serikali kutoa fedha kulingana na bajeti iliyopitishwa ili kutengeneza mazingira mazuri ya elimu kwa walimu na wanafunzi hivyo kuongeza ufanisi katika elimu na hatimaye kufanikisha malengo yaliyowekwa,” alisema CAG.

Elimu bila malipo ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/20 na ilianza kutekelezwa Januari 2016 ambapo Serikali imenukuliwa mara kadhaa ikisema inatumia zaidi ya Sh23.8 bilioni kila mwezi kugharamikia utekelezaji wake.

Kichere anasema amefanya tathmini ya utoshelevu wa miundombinu ya elimu hasa shule za msingi na sekondari katika halmashauri 30 na kubaini upungufu wa miundombinu ya elimu pamoja na walimu katika shule zote za msingi na sekondari hivyo kuathiri ubora wa elimu inayotolewa.

Hali ilivyo

Ripoti hiyo inaonyesha mahitaji ya madarasa ya sekondari kuwa ni 8,261 na yaliyopo 6,632, sawa na upungufu wa 1,629 (asilimia 20) wakati maabara zinahitajika 1,200 zilizopo ni 724 na pungufu ni 472 sawa na asilimia 40.

Kuhusu vyoo, ripoti inasema yanatakiwa mashimo 12,430 lakini yaliyopo ni 7,915 na pungufu ni 4,515 sawa na asilimia 36. Kwa mahitaji ya madawati CAG anasema ni 213,012 yaliyopo ni 176,477 na pungufu ni 36,535 sawa na asilimia 17.

Upungufu mkubwa uko katika nyumba za walimu ambazo zinatakiwa kuwa 13,292 lakini zilizopo ni 2,161 na pungufu ni 11,131 sawa na asilimia 84. Kwa upande wa shule za msingi, madarasa yanahitaji 35,979 na yaliyopo ni 19,119 na pungufu ni 16,860 sawa na asilimia 47.

Shule hizo za msingi zinahitaji vyoo 60,006 ila nilivyopo ni 25,669 na pungufu ni 34,337 sawa na asilimia 57. Madawati yanapaswa kuwa 417,141 lakini yaliyopo ni 339,580 ikiwa ni pungufu ya 77,561 sawa na asilimia 19.

Ripoti hiyo inaonyesha nyumba za walimu wa msingi zinahitajika 34,213 ila zilizopo ni 8,069 na pungufu ni 26,144 sawa na asilimia 76.

“Hali hii inaonyesha uhaba wa miundombinu ya elimu inayoweza kuathiri ubora wa elimu inayotolewa ambayo inaweza kusababisha matokeo mabaya ya wanafunzi,” anasema Kichere

Kwa mujibu wa CAG, madhumuni ya muda mrefu ya kutoa elimu bora hayawezi kufikiwa ikiwa hatua madhubuti hazitachukuliwa na Serikali.

“Kwa hiyo, ninazishauri halmashauri, kwa kushirikiana na Tamisemi, wizara ya elimu, sayansi na teknolojia na wadau wengine kuweka mikakati ya uboreshaji wa miundombinu iliyopo na kuanzisha miundombinu mipya ili kuboresha elimu nchini,” anasema

Halmashauri tano kitanzini

CAG amesema katika ukaguzi wake amebaini Sh101 milioni zilizotolewa na halmashauri tano kwa mikataba ambayo haikutelekezwa kama inavyopaswa na kushauri fedha hizo zirejeshwe vinginevyo wahusika wawajibishwe. Alizitaja halmashauri hizo na kiwango inachopaswa kurejesha ni Sumbawanga Sh60.86 milioni, Tabora Sh3 milioni, Monduli Sh10 milioni; Chunya Sh20 milioni, Nanyamba Sh7.14 milioni.

“Kwa maoni yangu, halmashauri hazikuwa makini kupima kazi zilizofanyika kabla ya kufanya malipo na kupelekea matumizi mabaya wa fedha za umma,” anaeleza.

“Ninapendekeza halmashauri zirejeshe Sh101 milioni kutoka kwenye hati za malipo zinazofuata. Vinginevyo, mameneja miradi husika wawajibishwe,” alisema.