VIDEO: CAG asema hali ya utekelezaji wa mapendekezo yanayotolewa hauridhishi

Thursday March 26 2020

By Peter Elias, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG), Charles Kichere amesema ofisi yake ilitoa mapendekezo 266 lakini ni mapendekezo 82 pekee ndiyo yametekelezwa kikamilifu wakati mapendekezo 95 utekelezaji wake ukiendelea, mapendekezo 65 hayajatekelezwa kabisa na mengine 22 yamepitwa na wakati.


Kichere amesema hayo leo Alhamisi Machi 26, 2020 kabla hajakabidhi ripoti yake kwa Rais John Magufuli.
"Hali ya utekelezaji wa mapendekezo yanayotolewa na CAG hauridhishi, kati ya mapendekezo 266 niliyoyatoa ni 82 pekee ndiyo yametekelezwa kikamilifu," amesema Kichere.


Kichere amesema huko nyuma mashirika mengi ya umma yalikuwa yakikaguliwa na taasisi binafsi kwa sababu ya uchache wa wafanyakazi.
Hata hivyo, amesema ofisi yake imekagua mashirika 10 ya umma ambayo yalikuwa yakikaguliwa na taasisi binafsi na kuifanya ofisi yake kuokoa Sh1.4 bilioni ambazo zilikuwa zikilipwa kama ada ya ukaguzi kwa taasisi binafsi.


Amesema katika mwaka wa fedha wa 2019/20, ofisi yake imepanga kuongeza ukaguzi kwa mashirika mengine 10 ya umma ambayo ni pamoja na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Shirika la Ndege  Tanzania(ATCL).


"Tukikamilisha ukaguzi wa mashirika haya, tutaokoa kiasi kingine cha Sh1.4 bilioni," amesema Kichere wakati akiwasilisha ripoti yake kwa Rais Magufuli.

Advertisement