CAG ataja sababu kuchelewa miradi

Dar es Salaam. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imezitaja sababu za ucheleweshaji wa ukamilishaji wa ujenzi wa shule na miradi ya maji ni Serikali kutotoa fedha za kutosha, wakandarasi wasio na uwezo na changamoto za usanifu wa michoro.

Mbali na hayo, ripoti hiyo pia imeeleza kuwa mapungufu yatokanayo na manunuzi pia yalikwamisha miradi hiyo kukamilika kwa wakati.

Katika sekta ya elimu, CAG alibaini ucheleweshaji wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Ihungo kwa miezi 24 na ucheleweshaji wa ukarabati wa Shule za Sekondari Azania na Jangwani kwa miezi 12 kinyume cha makubaliano yaliyosainiwa kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) yenye thamani ya Sh 12.9 bilioni.

CAG alibaini pia ucheleweshwaji kama huo kwenye sekta ya maji, ambapo miradi 65 inayotekelezwa na halmashauri 22 za mamlaka za Serikali za mitaa yenye thamani ya Sh bilioni 63.7 ilichelewa kukamilika kwa muda wa kati ya miezi mitatu hadi 48.

“Iwapo changamoto nilizozitaja hapo juu zingepatiwa ufumbuzi mapema ikiwamo kuwapo kwa wakandarasi wenye weledi kusingekuwa na ucheleweshwaji huo.”

“Ninahitimisha kwa kutambua na kupongeza jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali katika kuhakikisha kuna uwajibikaji mkubwa na utawala bora katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo,” amesema CAG katika ripoti hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma Aprili 10 mwaka huu.

Hata hivyo, CAG amesema kuwa kuna changamoto nyingi zinazokabili utekelezaji na hivyo kukwamisha mafanikio ya miradi.

Alisema kuna changamoto ambazo zipo ndani ya uwezo wa mamlaka ya maofisa masuuli katika kuzishughulikia na kuzitatua na nyingine hazipo ndani ya uwezo wa mamlaka ya maofisa hao.

“Kwa ujumla, nimebaini mapungufu katika usimamizi wa fedha, usimamizi na mikataba, udhibiti wa matumizi, pamoja na kutofuata matakwa ya makubaliano katika mikataba iliyosainiwa.”

“Masuala haya yanaathiri utekelezaji wa miradi nchini, katika taarifa hii nimeyaelekeza mapendekezo yangu kwa Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuhakikisha kuwa wanatekeleza miradi, kusimamiwa vizuri na kufuatiliwa katika kurekebisha mapungufu yaliyotajwa,” ilisema sehemu ya ripoti hiyo ya CAG.