CAG atoa agizo kwa Dawasa

Muktasari:

  • Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imebainisha kwamba Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka inatakiwa kulipwa fidia na mkandarasi wa mradi wa visima 20 vya Kimbiji na Mpera kwa kutokamilisha mradi huo kwa wakati kama ilivyobainishwa kwenye mkataba wao.

Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ameitaka Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (Dawasa) kudai fidia ya Sh1.98 bilioni baada ya mkandarasi kutokamilisha kwa wakati mradi wa visima 20 katika eneo la Kimbiji na Mpera jijini Dar es Salaam.

Katika ripoti yake ya ukaguzi kwa mashirika ya umma ya mwaka 2017/18, CAG amebainisha kwamba Dawasa ilitiliana saini na kampuni ya M/S Serengeti pia iliingia ubia na kampuni ya NSPT Ltd kwa ajili ya ujenzi wa visima hivyo kwa gharama ya Sh19.82 bilioni.

“Kifungu namba 8.7 cha mkataba kinabainisha kwamba, endapo mkandarasi hawezi kukamilisha kazi ndani ya muda uliokubaliwa, mkandarasi anapaswa kutozwa fidia kwa kuchelewa kukamilisha kazi kwa kiwango cha asilimia 0.05 ya bei ya mkataba, lakini isizidi asilimia 10 ya bei ya mwisho ya mkataba,” amebainisha CAG.

Amesema kwa mujibu wa mkataba huo (DAWASA/CW/2012-2013/10), kazi ilitakiwa kukamilika Disemba 31, 2015, hivyo, fidia ya kuchelewa kukamilisha kazi hiyo ilipaswa  kuombwa kuanzia Januari 1, 2016 kufikia kiwango cha juu cha asilimia 10, Julai 18, 2016 ikiwa ni siku 200 ambazo ni jumla ya Sh1.98 bilioni.  

“Dawasa ilipaswa kudai Sh1.98 bilioni ikiwa ni fidia inayotokana na kuchelewa kukamilisha mradi. Hata hivyo, Dawasa haikudai pesa hizo. Napendekeza Dawasa idai fidia hiyo kutoka kwa mkandarasi,” amesema.

Januari 24, 2019, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa alitembelea mradi huo na kumwagiza mkandarasi kumaliza kazi haraka. Profesa Mbarawa alisema visima 12 vya Kimbiji vilikuwa vimekamilika kilichobaki ilikuwa kupima wingi wa maji.