CCM Dar yatuma ujumbe kwa wanachama wake uchaguzi Serikali za mitaa

Tuesday October 22 2019

Katibu wa CCM Mkoa wa  Dar es Salaam, Zakaria

Katibu wa CCM Mkoa wa  Dar es Salaam, Zakaria Mwansasu 

By Tumaini Msowoya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Katibu wa CCM Mkoa wa  Dar es Salaam, Zakaria Mwansasu amesema wanachama wa chama hicho watakaobainika kupenya kwa rushwa katika kura za maoni  kuwania uongozi kwenye uchaguzi Serikali za mitaa hawatateuliwa.

Uchaguzi wa Serikali za mitaa unafanyika Novemba 24, 2019 na kwa sasa vyama mbalimbali  vya siasa vipo katika hatua ya kwanza ya uteuzi wa wagombea.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Oktoba 22, 2019 Mwansasu amesema uamuzi huo ni mwanzo wa kuanza kuyafanyia kazi maagizo ya katibu mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally.

Dk Bashiru ameagiza kurudiwa uchaguzi wa ndani wa kupata wagombea wa  CCM katika maeneo yenye  malalamiko.

Katika maelezo yake Mwansasu amesema kinachofanyika sasa ni kupitia malalamiko yaliyowasilishwa.

“Kwa sasa tunapitia malalamiko yote yaliyowasilishwa na wanachama walioomba kuteuliwa kuiwakilisha CCM. Baada ya maagizo tunaendelea kushughulikia, kufuatilia na kutekeleza kile alichoagiza.”

Advertisement

“Uchaguzi wa ndani ya CCM sio wa ushindani ni kura za maoni kwa hiyo mtu awe ameongoza, wa pili au watatu kama atabainika kura alizopata ni kwa hila au rushwa  hatafikiriwa katika uteuzi,” amesema.

Amebainisha kuwa wanachama wa chama hicho tawala nchini Tanzania wamepata mwamko wa kugombea na kupiga kura za ndani kuwapata wagombea wake wa uchaguzi huo.

 

Advertisement