CCM Mara kuzindua kampeni kesho kwa kuanza kuelezea mafanikio ya Serikali

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Sameul Kiboye

Muktasari:

Chama cha Mapinduzi (CCM ) kitazindua kampeni zake kesho, pia kinakusudia kupita kila wilaya kuzungumza na wananchi kuelezea mafanikio ya serikali ya awamu ya tano katika kipindi cha miaka minne

Musoma. Ikiwa leo ni siku rasmi ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa utakao fanyika Novemba 24 mwaka huu, Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mara kitazindua rasmi kampeni hizo kesho Jumatatu Novemba 18.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Sameul Kiboye akizungumza na MCL Digital amesema leo Jumapili Novemba 17, 2019 kuwa licha ya baadhi ya vyama vya upinzani kujitoa katika uchaguzi huo, lakini bado vipo vyama ambavyo vimesimamisha wagombea katika baadhi ya maeneo.

Amevitaja vyama vilivyosimamisha wagombea katika baadhi ya maeneo kuwa ni UDP, TLP Na Sauti ya Umma (SAU) huku chama hicho kikipita bila kupingwa katika maeneo yote wilayani Tarime.

Alisema kuwa kwa mujibubwa tathmini waliyofanya, chama cheke kimeshinda kwa zaidi ya asilimia 90 na kwamba kutokana na hali hiyo chama chake hakitakuwa na kazi  kubwa katika kutafuta ushindi katika baadhi ya maeneo yaliyosalia.

" Tunakwenda kushinda kwa kishindo kwa sababu tayari tuna ushindi mkubwa kwa hiyo hayo maeneo mengine tunaamini hakuna kikwazo chochote na tayari uongozi wa kila wilaya umeanza mchakato wa kampeni leo ingawa rasmi kimkoa tutaanza kesho,” amesema Kiboye.

Amesema kuwa kutokana na hali ilivyo chama chake kitajikita katika kueleza kile ambacho serikali ya chama chake kimefanya katika kipindi cha miaka minne ili wananchi waweze kuelewa kwa ufasaha zaidi na kuachana na upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu ambao amedai kuwa hawana nia nzuri.

Amefafanua kuwa mikutano ya kueleza mafanikio ya chama chake itafanyika katika kila wilaya bila kujali kama eneo husika wamepita bila kupingwa na kwamba kwa kufanya hivyo pia watakuwa wanawaandaa wananchi kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika mwakani.

“Kama ni kushinda sisi tumeshashinda lakini lazima tupite kila sehemu kueleza yale ambayo chama chetu chini ya Rais Magufuli kimefanya kwa sababu sisi tumejipanga baada tu ya kumaliza uchaguzi huu wa serikali za mitaa tunaanza rasmi maandalizi ya uchaguzi mkuu mwakani,” amesema Kiboye.