CCM ilivyoendesha kampeni kuzingatia maagizo ya Magufuli

Magufuli: CCM imefanya kampeni za kistaarabu

Muktasari:

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema viongozi na wagombea wa chama hicho wamefanya kampeni kwa kuzingatia maagizo makuu matatu waliyopewa na mwenyekiti wao, John Magufuli.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema viongozi na wagombea wa chama hicho wamefanya kampeni kwa kuzingatia maagizo makuu matatu waliyopewa na mwenyekiti wao, John Magufuli.

Bashiru amesema hayo leo Jumanne Oktoba 27, 2020 kwenye mkutano wa mgombea urais wa chama hicho alipozungumza na wazee na waandishi wa habari  jjijini Dodoma.

Amesema maagizo hayo yalilenga kulinda misingi ya utaifa wakati wote wa kampeni, hivyo  wamezingatia mambo hayo.

“Kwanza ulituambia tujikite katika hoja ya yale tuliyofanya vizuri miaka mitano iliyopita na yale tutakayoyafanya miaka mitano ijayo, kazi hiyo imefanywa vizuri sana na wewe (Magufuli) umetuongoza.

“Pia ulituelekeza tutumie lugha za kisraatabu na kiuungwana tusijibu matusi kwa matusi, bali matusi yajibiwe kwa hoja kazi hiyo tumeifanya. La mwisho tutengeneze mazingira ya kuwashawishi wapiga kura ili kesho 28 wajitokeze kwa wingi na wengi wao watupigie kura kazi hiyo pia tumeifanya,” amesema Bashiru.

Amesema maelekezo mengine ilikuwa ni nidhamu ya chama, utii wa maelekezo, mambo ambayo yamekamilishwa na kuongozwa na mgombea huyo wa urais na yametimizwa vizuri.