KALAMU HURU: CCM isipoangalia itaingia Uchaguzi Mkuu wa 2020 ikiwa na mpasuko

Wednesday July 17 2019

 

By Elias Msuya

Tamko la malalamiko lililotolewa na makatibu wakuu wastaafu wa CCM, Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana dhidi ya “mwanaharakati anayejitambulisha kuitetea Serikali” ni dalili ya mpasuko ndani ya chama hicho.

Katibu wa Baraza la ushauri wa viongozi wastaafu, Pius Msekwa amekiri kuyaopokea malalamiko hayo akiwaambia wahusika wajibu mapigo.

Mwanaharakati huyo pia kupitia vyombo vyake vya habari amewashutumu hata viongozi na makada wa vyama vya upinzani na watu wengine wanaoonekana kuikosoa Serikali. Kwa kuwa sasa makatibu hawa wamejitokeza hadharani kulalamika, huenda wakatoa mwanya kwa wengine wasiokuwa na majukwaa kupaza sauti zao.

Malalamiko haya yanakuja wakati tukielekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa baadaye mwaka huu na pia tunajiandaa na uchaguzi mkuu mwakani.

Hivi karibuni, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole aliwaambia waandishi wa habari kuwa chama hicho kitashinda kwa kishindo katika chaguzi hizo kuwa kimeshamaliza mpasuko uliokuwapo kwenye mikoa yenye nguvu ya upinzani.

Pengine Polepole aliyasema hayo bila kujua, kwani sasa mpasuko unaonekana upo kuanzia juu. Malalamiko ya wazee hao wastaafu na makada wengine wa CCM, yanahoji kwa nini mwanaharakati huyo hawajibishwi na uongozi wa chama?

Advertisement

Kwa kuwa mwanaharakati huyo amejibainisha kuitetea serikali na chama akiwashutumu makada, viongozi na wastaafu, basi malalamiko yao ni kwa uongozi wa chama na serikali.

Kama nilivyosema awali, malalamiko hayo yamekuja wakati mbaya, kwani huu ni wakati wa chama kujipanga kwa njia zote ili kushinda chaguzi zijazo. Ni pamoja na kuhakikisha chama kinajitenga na fitina, chokochoko na maudhi.

Kauli kwamba CCM itashinda kwa kishindo haina maana sana wakati kukiwa na manung’uniko mengi miongoni mwa wanachama ambayo hayana majibu.

Kwa mfano, hata suala la makada wa vyama vya upinzani wanaohamia CCM na kupewa vyeo harakaharaka nalo halijawahi kupatiwa majibu ya kueleweka. Mtu alikuwa akikitukana chama huko, ghafla akihamia tu anakuwa DC au katibu tawala au alikuwa mbunge upande wa upinzani, anahamia CCM na papo hapo kupitishwa kuwa mgombea bila hata kura ya maoni.

Kuna wana CCM wamekipigania chama hicho kwa muda mrefu na wanafuata taratibu zote lakini ukifika muda wa kupewa vyeo, wanapewa watu wa nje (wakuja). Ni suala linaloibua manung’uniko miongoni mwa wanachama.

Kama hiyo haitoshi, jeshi hilo limekuwa mstari wa mbele si tu kuzuia mikutano ya hadhara ya vyama vya upinzani, bali hata vikao vya ndani, wakati CCM wanafanya bila bugudha yoyote.


Advertisement