CCM wapita bila kupingwa vijiji 6,248

Muktasari:

  • Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa nchini Tanzania (Tamisemi), Selemani Jafo ametangaza wenyeviti wa vijiji 6,248, wa mitaa 1169 na vitongoji 37,505 wanaotokana na CCM wamepita bila kupingwa baada ya kutojitokeza kwa wagombea kutoka vyama vya upinzani.

Dodoma. Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Selemani Jafo amesema wagombea 6,248 kati ya 12,319 wanaotokana na Chama cha CCM wamepita bila kupingwa baada ya kutojitokeza kwa wagombea wa vyama vingine.

Akizungumza leo Jumapili Novemba 10, 2019, Jafo amesema pia wagombea uwenyekiti wa chama hicho 1,169  kati ya mitaa 4,263 sawa na asilimia 27 wamepita bila kupingwa.

“Kwa upande wa vitongoji Chama cha Mapinduzi kimepita bila kupingwa katika vitongoji 37,505 kati ya vitongoji 64,384 sawa na asilimia 58,” amesema.

Amesema katika wajumbe wa kundi la wanawake jumla ya wajumbe 64,085 wamepita bila kupingwa na wajumbe kundi la mchanganyiko jumla ya wajumbe 75,560 wamepita bila kupingwa.