CCM yampitisha Mtaturu kumrithi Tundu Lissu

Miraji Mtaturu

Muktasari:

Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) chini ya Mwenyekiti wake, Rais John Magufuli ameongoza kikao cha kamati hiyo leo Jumatano ambacho kimemteua Miraji Mtaturu kuwa mgombea ubunge wa Singida Mashariki katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Julai 31, 2019

Dar es Salaam. Chama tawala nchini Tanzania cha CCM kimemteua Miraji Mtaturu kuwa mgombea ubunge wa Singida Mashariki.

Taarifa iliyotolewa na katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole imesema kikao cha Kamati Kuu kimekutana leo Jumanne Julai 16, 2019 chini ya Mwenyekiti wake, Rais John Magufuli jijini Dodoma kikiwa na agenda moja.

Polepole amesema agenda hiyo ilikuwa ni ya maandalizi ya uchaguzi huo kwa kuteua jina la mgombea ambapo Mtaturu ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya (DC) ya Ikungi mkoani Singida ndiye aliyeteuliwa.

Uchaguzi katika jimbo hilo utafanyika Julai 31, 2019 kujaza nafasi iliyoachwa na Tundu Lissu ambapo ilielezwa na Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai kwamba amepoteza sifa.

Juni 28 mwaka 2019, bungeni jijini Dodoma, Spika Ndugai alilitangazia Bunge kwamba Lissu amepoteza sifa za kuwa mbunge kutokana na sababu mbili ya kutokuhudhuria vikao vya Bunge pasina kutoa taarifa kwake  na kutokujaza fomu za mali na madeni ya viongozi wa umma.

Tayari Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza ratiba ya uchaguzi wa jimbo hilo ambapo fomu za kuomba kuteuliwa zimeanza kutolewa Julai 13 hadi 18 mwaka huu na kampeni zitakuwa Julai 19 hadi Julai 30 kisha  uchaguzi Julai 31, 2019.