CCM yasema mawazo ya Karume bado yanaishi

Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar Dk Abdalla Juma Saadala

Muktasari:

Kiongozi wa CCM visiwani Zanzibar, Dk Abdalla Juma Sadalla amesema mawazo ya mzee Abeid Amani Karume bado yanaishi.

Dar es Salaam. Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar Dk Abdalla Juma Saadala amesema ingawa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume alifariki miaka 48 iliyopita, mawazo yake bado yanaishi.

Dk Sadalla amesema hayo leo Jumanne, April 7, 2020 wakati wa akizungumzia kumbukizi ya kifo cha kiongozi huyo visiwani Zanzibar.

“Alikuwa na sifa ya kujishusha na sifa ya kutawala katika Serikali shirikishi, kwa hiyo leo ni siku muhimu sana kwetu ni kweli hayupo lakini mawazo yake na hekima zake zinaendelea kudumishwa milele na milele,” amesema Dk Abdalla.

Amesema hayati Karume ni kati ya viongozi walioithibitishia dunia kwamba Waafrika wanaweza kujitawala.

“Amethibitisha kuwa sisi Waafrika, tunaweza kuungana na kujitawala, kuweka uchumi wa Taifa na kudumisha Amani na umoja wa nchi yetu,” amesema.

Kiongozi huyo wa CCM Zanzibar amesema Karume alisaidia kuleta maendeleo ya Zanzibar na alitamani kuona kila mwananchi anafaidika na matunda ya nchi yake.

“Alitaka kusiwe na kero ya matabaka baina ya mtu mmoja na mwingine na aliandaa wizara maalum ya kuweka hali za wananchi sawa,” amesema.

“Aliacha usia mzuri na viongozi wengine waliofuatia wamekuwa wakitekeleza awamu kwa awamu kwa hekima kubwa sana.”