CCM yataka Zimbabwe kuondolewa vikwazo

Muktasari:

Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania kimeitaka jumuiya za kimataifa kuondoa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Zimbabwe bila masharti yoyote.


Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania kimeitaka jumuiya za kimataifa kuondoa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Zimbabwe bila masharti yoyote.

Kimesema Zimbabwe inapaswa kupiga hatua za haraka za maendeleo, uchumi na kijamii kwa watu wake.

Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi Oktoba 24, 2019 na makamu mwenyekiti wa CCM (Bara), Phillip Mangula katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Amesema CCM kinaamini vikwazo dhidi ya Zimbabwe ni mwendelezo wa fikra na matendo ya uonevu na unyanyasaji kwa Waafrika.

CCM imetoa kauli hiyo kipindi ambacho Marekani imemwekea vikwazo balozi wa Zimbabwe nchini Tanzania, Anselem Sanyatwe kwa tuhuma za kuwaamuru wanajeshi wa nchi hiyo kuwafyatulia risasi za moto waandamanaji waliokuwa wakipinga kitendo cha Tume ya uchaguzi Zimbabwe kuchelewa kutangaza matokeo.

Katika uchaguzi huo Rais Emmerson Mnangagwa aliibuka mshindi wa kitu cha urais.

“Watu wa Zimbabwe wameonewa kiasi cha kutosha na sasa tunaazimia kuwa uonevu huo ufike mwisho,” Amesema Mangula.

Kauli kama ya Mangula imewahi kutolewa na mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli katika mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc).

Katika maelezo yake Mangula amesema, “kwa kutambua jukumu letu katika kuimarisha umoja, mshikamano wa Waafrika na kuendeleza mapambano dhidi ya ukoloni mamboleo, kupiga vita ubeberu na ubaguzi wa aina yoyote pamoja na kuimarisha uhusiano mwema CCM kama ilivyo vyama vingine ni lazima ikatae dhuluma zinazoendelea dhidi ya Zimbabwe.”

Amesema CCM inaungana na maazimio ya mkutano wa 10 wa vyama vya ukombozi  vya nchi za Sadc.

“Kwa tamko hili tunaweka msisitizo na kupitia kwa Serikali za Tanzania, Sadc na Afrika Mashariki (EAC) kwamba ifike wakati Umoja wa Afrika uchukue nafasi yake na kusimamia haki za wanachama ambao  wanaendelea kuonewa kwa nguvu za kibeberu na ukoloni mamboleo,” amesema Mangula.

Alisema CCM inatambua juhudi zilizofanywa na Serikali ya Zimbabwe ikiwamo kuimarisha demokrasia na uongozi bora pamoja na kujitegemea kiuchumi.

Amesema kutokana na vikwazo hivyo,  nchi hiyo inashindwa kupiga hatua za maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kasi inayostahili.

Awali balozi huyo wa Zimbabwe nchini ambaye alihudhuria mkutano huo wa CCM, amesema kuendelea kuiwekea vikwazo nchi yake siyo sawa kwa kuwa wanaoumia ni wananchi.

“Zimbabwe iliwekewa vikwazo tulipofanya mageuzi ya ukombozi ambako tulibadili sera ya umiliki wa ardhi kwa asilimia 75 iliyokuwapo ikimilikiwa na Waingereza ikarejeshwa kwa wenyeji hili hakikuwafurahisha wakatushtaki katika Umoja wa Ulaya (EU).”

“EU ikatuwekea vikwazo na baadaye vikazidi mpaka Marekani pia wakatuadhibu. Hii siyo sawa sasa miaka zaidi ya 19 imepita wanaathiri vizazi vipya hata wale waliosababisha wengine washakufa,” amesema balozi Sanyatwe.