CCM yatangaza mchakato kuandaa sera, ilani ya uchaguzi 2020/25

Tuesday December 31 2019

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Dar es Salaam. Chama Cha Mapinduzi (CCM) nchini Tanzania kimesema kiko katika mchakato wa kuandika mwelekeo wa sera za CCM kwa mwaka 2020 hadi 2030 pamoja na uandaaji wa Ilani ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020/2025.

Taarifa iliyotolewa leo Jumanne Desemba 31, 2019 na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole imesema katika michakato yote ya uandaaji nyaraka muhimu za chama ikiwamo mwelekeo wa sera na Ilani huwa ni ushiriki na ushikishaji wa umma wa Watanzania na wanachama wa CCM kote nchini.

Amesema msingi huu wa kushirikisha umma unatokana na asili ya chama ya Chama Cha Mapinduzi ambayo ni vitu viwili, kutenda haki na kuheshimu watu.

“Chama kinawakaribisha mtu mmoja mmoja au vikundi vya watu na taasisi mbalimbali ikiwamo lakini si kwa uchache, vyama vya wafanyakazi, wawakilishi na vyama vya wakulima, vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, vyama vya waalimu, wachimbaji wadogo wadogo wa madini,” amesema Polepole

Vingine ni, wafanyabiashara wa madini, wawakilishi na vyama vya wakulima, wavuvi na wafugaji, jumuia za wamachinga na wasafirishaji wadogo wadogo, bodaboda na bajaj.

Polepole amesema jumuia za wanawake, watu wenye ulemavu, vijana, wazee, watoto, Asasi Zisizokuwa za Kiserikali (AZISE), wasomi, wanafunzi wa vyuo na vyuo vikuu, wadau na wana tasnia ya sanaa, burudani na michezo, wasafirishaji wa mizigo na abiria, wenye viwanda, wadau wa sekta ya utalii na vyama vya ushirika kwa maeneo yao.

Advertisement

Amesema kwa wanachama wa CCM kamati za siasa za mikoa na wilaya ziweke utaratibu wa kukusanya maoni na kuwasilisha makao makuu kama ambavyo imekwisha kuelekezwa.

“Kamati ya Uandishi wa Mwelekeo wa Sera na Ilani ya CCM chini ya Mwenyekiti wake Mzee Phillip Mangula Makamu wa Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara inaomba maoni haya yawe yamefika kwa Kamati kabla ya Januari 25, 2020,” amesema Polepole .

Amesema maoni yanaweza kuwasilishwa kwa Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally, au kwake (Polepole).

“Uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya John Magufuli, mwenyekiti wa CCM na Rais wa Tanzania unapenda kuwatakia wana CCM na Watanzania wote Heri ya Mwaka Mpya, Mwaka 2020 ukawe wenye baraka, amani, umoja, neema, mafanikio na kuinuliwa kwa mtu mmoja mmoja na Taifa la Tanzania, sote tukafanye kazi kwa bidii na huu ukiwa ni msingi wa kulinda utu na uhuru wa Taifa letu,” amesema

 

Advertisement