CCM yatoa maagizo matano ya lala salama

Katibu Mkuu wa Chama Chas Mpainduzi (CCM), Dk Bashiru Ally

Muktasari:

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally, ametoa maagizo matano kwa wagombea na viongozi wa chama hicho, ikiwa zimebaki siku za lala salama kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28.

Mwanza. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally, ametoa maagizo matano kwa wagombea na viongozi wa chama hicho, ikiwa zimebaki siku za lala salama kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28.

Ni maagizo yanayoashiria mikakati ya chama hicho tawala kufanya vizuri katika uchaguzi huo.

Akizungumza na wanachama na wafuasi wa CCM jijini Mwanza jana, Dk Bashiru aliwaagiza viongozi na makada wa chama hicho kubadilisha mbinu na mashambulizi ya ushindi kwa kujielekeza katika utoaji elimu kwa wapigakura, badala ya kung’ang’ania kuendelea kueleza utekelezaji wa miradi na ahadi.

Aliwaeleza waliohudhuria mkutano huo uliofanyika uwanja wa CCM Kirumba kuwa taarifa za utekelezaji na ahadi ziko kwenye ilani na zimefafanuliwa kabla na wakati wote wa kampeni.

“Sasa tubadilishe maudhui ya kampeni zetu kwenye majukwaa kwa kujielekeza zaidi kwenye kuwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi na namna ya kupiga kura kwa usahihi bila makosa,” alisema.

Maagizo mengine aliyoyaelekeza kwa watendaji na wajumbe wa sekretarieti za CCM kuanzia ngazi ya kata, wilaya na mikoa ni kutambua vituo vya kupigia kura, kuwatambua mawakala wenye uwezo na weledi na kuwaandaa kusimamia vema shughuli ya kupiga kura na kulinda maslahi ya chama hicho vituoni.

“Ofisi yangu tayari imetoa fedha kwa kila mkoa kwa ajili ya posho za mawakala. Fedha hizo zikiliwa mratibu wa mkoa husika atakiona cha moto,” alisema na kuonya Dk Bashiru

Utii wa sheria

Mtendaji huyo mkuu wa CCM pia aliwaagiza wagombea na viongozi wa chama hicho kuheshimu na kutii sheria, kanuni na miongozo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ikiwamo katazo la vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani na usalama.

“Tuwaelekeze na kuwazuia wapenzi, wafuasi wa CCM na wagombea kutofanya fujo wala kujichukulia sheria mikononi; tusifanye kazi ya Jeshi la Polisi, Mahakama au NEC. Tunapobaini kuwapo kwa viashiria vya uvunjifu wa amani tutoe taarifa kwa vyombo na mamlaka husika,” alifafanua.

Siku ya kupiga kura

Katibu mkuu huyo pia aliwataka wagombea na viongozi wote wa chama hicho kuwaelimisha wanachama na wafuasi wao kutii sheria ya uchaguzi inayozuia uvaaji wa sare za chama, kubeba mabango sambamba na picha za mgombea siku ya uchaguzi.

Kitanzi kwa viongozi

Makatibu CCM wilaya na mikoa nao wamepigwa marufuku kupanda kwenye majukwaa ya kampeni kunadi wagombea, badala yake, wameagizwa kutumia muda wao mwingi kupanga na kutekeleza mikakati ya ushindi.

“Kazi ya kuwanadi wagombea sasa ifanywe na makatibu wenezi, makada wengine pamoja na wagombea wenyewe,” aliagiza Katibu mkuu huyo

Katika kufikia malengo ya ushindi, Dk Bashiru aliwaonya watendaji wa chama hicho ambao maeneo yao hayatafikia malengo ya ushindi katika uchaguzi kuwa wajiandae kuachia ngazi.