CTI yaipongeza Serikali kuifanya Tanzania ya viwanda

Mkurugenzi Mtendaji wa CTI, Leodegar Tenga

Muktasari:

Viongozi wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) walitumia hotuba yao kuelezea namna walivyogushwa na miradi mikubwa inayoendelea hivi sasa na Serikali ya Tanzania. CTI walisema hayo katika hafla ya tuzo za Rais kwa mzalishaji bora wa mwaka 2018 zilizofanyika jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Shirikisho la Wenye Viwanda Taznania (CTI) limesema linaunga mkono juhudi za Serikali za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda huku likipongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali kuboresha miundombinu na upatikanaji wa nishati.

Hayo yamebainishwa jana Alhamisi Oktoba 17, 2019 katika hafla ya tuzo za Rais kwa wazalishaji bora wa mwaka jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa CTI, Leodegar Tenga alisema wanachama wote wa CTI wanaunga mkono mpango huo wa Serikali wa kuwa na uchumi wa viwanda.

"Hali ya kuwa na viwanda vingi na vya kutosha itaongeza ushindani katika soko la ndani na nje," alisema.

Katika hafla hiyo ambayo mgeni Rasmi alikuwa Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa, Mwenyekiti wa CTI, Subhash Patel alisema uboreshaji wa miundombinu unaoendelea utapunguza gharama za uzalishaji wa bidhaa.

"Mradi wa umeme wa Stiglers Gorge na ule SGR ikikamilika itapunguza gharama za uzalishaji wa bidhaa hapa nchini hivyo kutakuwa na ustawi," alisema.

Alisema muhimu ni Watanzania kuongeza thamani katika kila bidhaa kwani kufanya hivyo kunaongeza manufaa na kutoa ajira.

Subhash alisema Taifa litaukumbuka uongozi uliopo madarakani sasa kutokana na kazi iliyofanyika.

Hata hivyo, alisema bado kunachangamoto ya malipo ya VAT kwa bidhaa ya sukari ya viwandani (VAT Refunds) huku akisema hilo limekuwa no tatizo kubwa.

Mshindi wa Jumla katika tuzo hizo ni Kampuni ya Hanspaul ya jijini Arusha ilitwaa tuzo tatu na kuibuka kuwa mshindi wa jumla wa tuzo hizo kwa mwaka 2018.

Hanspaul vinamiliki viwanda vya utengenezaji wa bidhaa za karatasi kama maboksi ya kufungashia bidhaa pamoja na utengenezaji wa magari maalumu ikiwemo kuyabadilisha muundo.