CUF wajitoa uchaguzi Serikali za mitaa

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba akizungumza na wanahabari leo Novemba 24, 2019.

Muktasari:

  • Chama cha Wananchi (CUF) kimejitoa katika uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019.

Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF) kimejitoa katika uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019.

Kimesema sababu za kujitoa ni kutoridhishwa na mwenendo wa mchakato huo ikiwa ni pamoja na asilimia 90 ya wagombea wake kuenguliwa.

Msimamo huo umetangazwa leo Jumanne Novemba 12, 2019 na mwenyekiti  wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba wakati akitoa maazimio ya kikao cha baraza kuu la uongozi la CUF.

CUF kinakuwa chama cha siasa cha sita kujitoa katika uchaguzi huo baada ya Chadema, ACT-Wazalendo, NCCR-Mageuzi, UPDP na Chauma.

Katika maelezo yake Profesa Lipumba amesema  baraza hilo limetafakari kwa kina na kuona hakuna umuhimu kushiriki uchaguzi baada ya hoja zao tatu walizoziwasilisha serikalini kutofanyiwa kazi.

" Uchaguzi unatakiwa uwe huru na haki lakini Serikali imeshindwa kuonyesha hata chembe ya haki. Asilimia 90 ya wagombea wetu wameondolewa tumebaki na asilimia nne tu.”

“Kwa mazingira haya ni wazi CUF imeondolewa,  hatuna namna zaidi ya kung'atuka,  hatuwezi kushiriki bila wagombea," amesema Profesa Lipumba.

Profesa Lipumba amewataka asilimia nne ya wagombea wa chama hicho waliopitishwa kugombea kujitoa na kuiomba Tamisemi kutotumia nembo ya chama hicho kwenye uchaguzi huo.