Cecil Mwambe arejea CCM

Muktasari:

Mbunge wa Ndanda (Chadema), Cecil Mwambe amejiuzulu  uanachama wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania na kujiunga na CCM leo Jumamosi Februari 15, 2020.

Dar es Salaam. Mbunge wa Ndanda (Chadema), Cecil Mwambe amejiuzulu  uanachama wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania na kujiunga na CCM leo Jumamosi Februari 15, 2020.

Mwambe ambaye takribani miezi  miwili iliyopita alijitosa kugombea uenyekiti wa Chadema akichuana na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ametangaza uamuzi huo mbele ya katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole. Katika uchaguzi huo Mwambe alishindwa na Mbowe.

Akizungumza kuhusu uamuzi wake huo Mwambe amesema vyama vya upinzani nchini vina safari ndefu ya kujenga demokrasia ya kweli, ameona  atakuwa anajidanganya na kuwadanganya wapiga kura wake kubaki katika vyama vya namna hiyo wakati bado anatamani kuwatumikia wananchi wa Ndanda.

“Leo kwa kuamua mwenyewe nimeamua kujiunga na CCM kama mtanipokea na kunikaribisha basi nipewe tena nafasi ya kugombea endapo mtaridhia na nitapata nafasi,” amesema Mwambe.

SOMA ZAIDI

Mwambe ambaye alijiunga  Chadema mwaka 2015 akitokea CCM ambako jina lake lilikatwa katika mchakato wa kura ya maoni kuwania kupitishwa kugombea ubunge, amesema ndani ya Chadema hakuna uwazi  katika suala la mapato na matumizi na wanachama hawana nafasi ya kuhoji lakini wanaonufaika ni wachache.

Paia amesema uamuzi wake wa kugombea uenyekiti na Mbowe uliibua chuki na laianza kuandamwa.

Naye polepole amesema Mwambe ametumia haki yake ya kikatiba na hivi karibuni waziri mkuu wa zamani, Frederick Sumaye alifanya hivyo kwa kurejea CCM.

Polepole amemhakikisha Mwambe kwamba katika chama anachojiunga uwazi wa mapato na matumizi upo wa kiwango cha juu na kila kitu kipo kielektroniki na kwa zaidi ya miaka miwili kimepata hati safi.

“Karibu sana  nitawafahamisha viongozi wakuu wa juu wa chama kuu nia yako njema,” amesema Polepole.

Alichokisema Magufuli kuhusu Mwambe

Oktoba 15, 2019 Rais wa Tanzania, John Magufuli alisema 'figisu' ndani ya CCM  zilisababisha  Mwambe kugombea ubunge wa Ndanda kwa tiketi ya Chadema.

Alieleza hayo aliposimama njiani kuzungumza na wakazi wa Ndanda wakati akielekea Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.

“Mbunge wenu huyu (Mwambe)  alikuwa mgombea wa CCM (mwaka 2015) anakubalika lakini kwa sababu ya figisu za watu wa huku (CCM) nataka nieleze ukweli mimi huwa napasuaga   tu wakaacha kumpitisha akaamua kuhama CCM."

"Kwa hiyo huyu ni wetu mlifanya makosa wenyewe na mnafahamu makosa ya kukosea kuchagua,” amesema Magufuli.

Amesema Mwambe alitakiwa awe mbunge wa CCM, alimuita mbunge huyo  azungumze kuhusu suala hilo.

SOMA ZAIDI

Katika maelezo yake Mwambe amesema, "niligombea kupitia CCM mwaka 2015 niliongoza kura za maoni kwa kuwa nilikuwa sifahamu mfumo mzuri wa chama kipindi hicho kura zangu alipewa mtu mwingine na niliambiwa kura zangu hazikutosha.”

 “Lakini Mungu alichagua niwe kiongozi wa Ndanda,  nilikwenda Chadema  nikashinda,  nina ahidi nitaendelea kushirikiana na wananchi wa hapa."

Baada ya Mwambe kueleza hayo Rais Magufuli amesema,  "wakati mwingine tunajicheleweshea maendeleo sisi wenyewe. Mtu anapendwa na wananchi, anakipenda chama lakini figisu za chama mnamnyima mtu anayetaka kushiriki. Hili liwe fundisho kwa wanachama na wananchi wa huku.”

“Mimi niligombea (waliojitokeza kupitishwa kuwania urais CCM mwaka 2015) na watu 42 wa CCM ila kiukweli mimi nilikuwa nakubalika hawakunifanyia mzaha wakanipitisha. Wanaokubalika msiwafanyie figisu hiki ni chama chetu wote.”

Ameongeza, "nimekusikia hata ninapokuona moyo wako umejaa CCM ninakuamini na kama upo tayari kuhamia CCM uhamie,  msimkate tena ninahitaji watu watakaonipa ushauri mzuri kwa kuwa tunaongea lugha moja inayofanana kama ilivyo kwa Nape (Nnauye-mbunge wa Mtama- CCM)."