Chadema Jiji la Arusha yapata viongozi wapya

Mwandikishaji wapiga kura kituo cha Ngateu wilaya ya ArumeruTemu Regan alisubiri watu kujitokeza kujiandikisha katika uchaguzi serikali za mitaa.katika kituo  hicho. Picha Mussa Juma

Muktasari:

Hatimaye Chama cha demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeanza kufanya chaguzi zake ngazi za wilaya, siku chache baada ya msajili wa vyama vya siasa kutishia kukichukulia hatua chama hicho kwa kuchelewa kufanya chaguzi.

Arusha. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika Jiji la Arusha kimepata viongozi  wapya baada ya Ephata Nanyaro kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa wilaya Arusha Jiji huku  Maxmiilian Malongo akichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la vijana na Witness Liwa kuwa mwenyekiti wa Baraza la wanawake.

Katika uchaguzi huo uliofanyika leo Jumapili Oktoba 13, 2019 katika ukumbi wa Safari hoteli na kusimamiwa na Katibu wa Idara ya uenezi makao makuu Chadema, Hemedy Ally na Katibu wa mkoa wa Chadema, Elisa Mungure, Nanyaro ambaye ni Diwani wa Levolosi, ameshinda uchaguzi huo baada ya kupata kura 96.

Nanyaro amemshinda  Elisante Akyoo aliyepata kura 38  na aliyekuwa Mwenyekiti wa wilaya, Derrick Magoma alijitoa pamoja na Edward Mollel na katika nafasi ya katibu,  Innocent Kisanyage amechaguliwa tena baada ya kupata kura 106 na kumshinda Regnald Masawe aliyepata kura 38. 

Akitangaza matokeo hayo, Mungure amesema nafasi ya Katibu mwenezi wa wilaya ameshinda Boniface Kimario  aliyepata kura 91  na kuwashinda  wagombea wengine watatu  na nafasi ya mweka hazina wa wilaya ameshinda Jafari ole Koimere kwa kupata kura 84 dhidi ya kura 65 za Mawazo Mathias.

Mungure amesema wajumbe wa mkutano mkuu, walioshinda ni Diwani wa Moiraro, Ricky Mairo aliyepata kura 59 na kumshinda Diwani wa unga limited, Wakili James Lyatuu aliyepata kura 40 na Emmanuel  Nyaki kura 47.

Katika baraza la vijana Jiji la Arusha, Maximillian Balongo ameshinda dhidi ya wagombea  watatu baada ya kupata kura 31 huku Katibu wa Bavicha, Emma Kimambo akishinda kwa kura 36 dhidi ya John William aliyepata kura 18.

Katika uchaguzi huo, Lucy Joel ameshinda nafasi ya uenezi Bavicha huku  Hussen Juma akishinda nafasi ya mweka hazina na Baraza la Wanawake, Witness Riwa amemwangusha Naibu Meya wa Jiji, Viola Likindoki baada yapata kura 51.

Nafasi ya Katibu mwenezi Bavicha, Veronica Mwilenge ameshinda na nafasi ya mwenyekiti wa Baraza la Wazee wilaya aliyeshinda ni Emmanuel Laisangai.

Akizungumza baada ya matokeo hayo, Mungure amewataka viongozi walioshinda kukiimarisha chama hicho lakini pia akawataka walioshindwa kuendelea kuwa na mshikamano na viongozi wapya ili kufanya vizuri katika chaguzi zijazo.