Chadema: Kuna wengine watamfuata Dk Mashinji

Katibu wa itikadi na uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole akimkaribisha Aliyekuwa katibu mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Vicent Mashinji leo Jumanne Februari 18, 2020 katika ofisi ndogo za CCM mtaa wa Lumumba.

Muktasari:

Chama cha Demokrasia na Maendeleo nchini Tanzania (Chadema) kimesema baada ya aliyekuwa katibu mkuu wake, Dk Vicent Mashinji kujiunga CCM, wapo wanachama wa chama hicho watakaomfuata.

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo nchini Tanzania (Chadema) kimesema baada ya aliyekuwa katibu mkuu wake, Dk Vicent Mashinji kujiunga CCM, wapo wanachama wa chama hicho watakaomfuata.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Februari 18, 2020 Mkurugenzi wa Itikadi, Uenezi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema, “Dk Mashinji tulimjua kuwa alikuwa amepanga safu ya mgombea wake wa uenyekiti (wa Chadema) ambaye ni  Mwambe (Cecil-alirejea CCM juzi akitokea Chadema).”

“Mgombea wake wa urais ambaye ni Sumaye (Frederick- waziri mkuu wa zamani)  naye amerudi CCM, sekretariati aliyokuwa ameiandaa nayo itaondoka Chadema ni suala la muda tu.”

Sumaye naye alirejea CCM baada ya kujiunga Chadema mwaka 2015.

Dk Mashinji amejiunga CCM leo katika ofisi ndogo za chama hicho zilizopo mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam ikiwa imepita miezi miwili tangu ufanyike mkutano  mkuu wa Chadema na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kutompendekeza tena kuwa katibu mkuu.

Badala yake, Mbowe alimpendekeza mbunge wa Kibamba, John Mnyika kuwa katibu mkuu wa tano wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania.

Baada ya kukosa nafasi hiyo, Dk Mashinji alieleza masikitiko yake kwamba alitamani kuendelea kuwa katibu mkuu ili aweze kumalizia mipango aliyokuwa nayo, ikiwemo maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2020.

Mrema akizungumzia kuondoka kwa Dk Mashinji amesema, “tunamtakia kila la kheri kwa uamuzi wake huo. Kuondoka kwake hakutakuwa na athari yoyote, kama aliondoka Dk Willbrod Slaa aliyekuwa katibu mkuu kwa miaka kumi tena wakati wa uchaguzi mkuu 2015  itakuwa yeye aliyekaa ofisini kama miaka miwili na ushehe.”

Mrema amesema si Dk Mashinji pekee bali kuna viongozi wengine wa chama hicho nao wataondoka kwa kuwa wana taarifa zao hasa waliokuwa wamejipanga kugombea na kushindwa kwenye uchaguzi wa ndani wa chama hicho uliofanyika Desemba 18 2019 katika ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam.