Chadema kuanza mikutano ya hadhara Tanzania nzima kuanzia Aprili 4

Muktasari:

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ametangaza kuanza kwa mikutano ya hadhara ya chama hicho kuanzia mwezi ujao akiwataka viongozi wake kujiandaa.

Dar es Salaam.Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ametangaza kwamba kuanzia Aprili 4 mwaka kuu wataanza mikutano ya hadhara Tanzania nzima akiwataka viongozi wa chama hicho kujiandaa na mchakato huo.

Mbowe ambaye ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Machi 16, 2020 wakati akizungumza na wanahabari ikiwa siku chache baada ya kutoka gereza la Segerea.

“Kwa kauli hii nawatangazia viongozi wote wa kanda, mikoa, wilaya, vijiji, vitongoji hadi mitaa kufanya mikutano ya hadhara kwa utaratibu uliopo kisheria. Tutadai vitu viwili tume huru na maandalizi ya uchaguzi mkuu.

"Nategemea wenye mamlaka wataingia busara kwa azimio langu la leo linaweza kuzingatiwa. Lakini subira yetu, uvumilivu wetu, upole umedhauliwa vya kutosha. Tumekuwa waungawana sana kutafuta maridhiano lakini wenye mamlaka wanatubeza," amesema Mbowe.