Chadema wachangishana fedha usiku kuwatoa kina Mbowe rumande

Muktasari:

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewahamasisha wanachama wake kuchanga Sh350 milioni kwa ajili ya kuwalipa faini viongozi wanane wa chama hicho waliotiwa hatiani leo Jumanne Machi 10, 2020 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu katika mashtaka 12 kati ya 13 yaliyokuwa yanawakabili.

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewahamasisha wanachama wake kuchanga Sh350 milioni kwa ajili ya kuwalipa faini viongozi wanane wa chama hicho waliotiwa hatiani leo Jumanne Machi 10, 2020 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu katika mashtaka 12 kati ya 13 yaliyokuwa yanawakabili.

Uamuzi wa kuwatia hatiani umetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba baada ya kupitia ushahidi wa upande wa mashtaka na ule wa utetezi.

Mbali na Mbowe na aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji, washtakiwa wengine ni Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika; Naibu Katibu Mkuu Salum Mwalimu (Zanzibar), Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.

Pia wamo mbunge wa Tarime mjini, Esther Matiko; Halima Mdee (Kawe); Esther Bulaya (Bunda) na John Heche (Tarime Vijijini).

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo jioni makamu mwenyekiti wa Chadema (Zanzibar), Said Issa Mohammed amesema hukumu hiyo ni dhuluma ya demokrasia na wapo tayari kukata rufaa na watanunua haki yao.

"Mtakumbuka tangu 2018 kulikuwa na kesi ya kubambikia viongozi wetu. Baada ya ushahidi tulikwenda mahakamani tukijua tutashinda," amesema Mohammed.

Amesema Chadema wataendelea na mapambano  na kwamba hadi leo saa 6 usiku wanataka wawe wamepata fedha hizo.

"Hukumu imetolewa saa 10 wakijua benki zote zimefungwa viongozi wetu wabaki. Ikifika kesho twende tukawatoe viongozi wetu. Tunao mawakili tutakata rufaa. Tutahakikisha tunafikia lengo saa 6 usiku," amesema.

Amewataka wanachama wao kutumia akaunti ya CRDB yenye jina la Chadema M4C 01J1080100600 na namba za mkurugenzi wa fedha, Rodrick Lutembeka 0754275531 na 0655 275 531 kufanikisha mchango huo.

Akihamasisha michango hiyo, Mwenyekiti wa Kanda ya Kati, Lazaro Nyalandu amesema hukumu hiyo ilikuwa ni jaribio la kidemokrasia ambalo wamelishinda.

"Nasimama hapa kwa sababu mwenyekiti wetu hatalala kwake, viongozi wetu hawatalala kwao kwa kupigania haki.

Tutasonga mbele, kufikia kesho saa 2 asubuhi tuwe tumefanikiwa," amesema Nyalandu.

Amewaomba Watanzania wa vyama vyote na wapenda demokrasia kuchangia faini hiyo.

"Wale ambao wamefurahi kwa kuumizwa kwa kina Mbowe na watakwenda kunywa soda na bia wajue tutashinda."

Naibu Katibu mkuu (Bara), Benson Kigaila amesema michango hiyo ina lengo la kuonyesha Serikali mshikamano wao.

"Tuwaonyeshe Serikali waliowaweka viongozi wetu ndani. Tuwaonyeshe, tukalipe hiyo hela, tuchange kila hela. Tunao wanachama milioni saba Kaskazini, Kusini, Kati na Magharibi na Mashariki tuchange. Kesho kabla ya misa ya kwanza wawe wametoka," amesema Kigaila.