Chadema yahofia wapiga kura kutoandikishwa

Msemaji wa Chadema kanda ya Pwani, Gerva Lyenda akizungumza na waandishi wa habari leo Dar es Salaam.

Muktasari:

Uboreshaji wa taarifa za wapiga kura kwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani unaendelea na unatarajiwa kufikia ukomo Februari 20.

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Pwani kimeitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuongeza siku za uboreshwaji wa taarifa za wananchi katika Daftari la Kudumu la wapiga kura katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Februari 18 jijini Dar es Salaam, msemaji wa Chadema Kanda ya Pwani, Gerva Lyenda amesema kuna hatari ya zaidi ya watu milioni tatu wasiandikishwe kutokana na kukosekana hamasa katika zoezi hilo.

"Mwaka 2015 katika mkoa wa Dar es Salaam waliandikishwa watu zaidi ya milioni 2.77, mkoa wa Pwani waliandikishwa watu 697,533. Jumla watu milioni 3.46 walioandikishwa," amesema Lyenda.

Ameongeza: "Kwa utafiti tulioufanya tunatarajia mwaka huu kutakuwa na ongezeko la asilimia 25 ya watu wenye sifa ya kuandikishwa, hivyo watafikia watu milioni 4.31, lakini mpaka sasa wameandikishwa watu chini ya milioni 1.5 na zimebaki siku chache."

Amesema hali hiyo imetokana na kutofanyika kwa uhamasishaji wa kutosha.

"Sisi Chadema tulitoa barua katika makanisa na misikiti Dar es Salaam na Pwani tukiwasihi viongozi wa dini wawahamasishe wauminj wao wakajiandikishe. Hata viongozi wetu wanafanya hamasa," amesema Lyenda.

"Tunaiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi iongeze siku watu wajiandikishe maana raha ya mchezo ni mashabiki."

Katika hatua nyingine, Lyenda ameitaka NEC kutokubali kuingiliwa na viongozi wa vyama vya siasa huku akiwataja mawakala wa CCM.

"Mawakala wetu wanabishana na mawakala wengine hasa wa CCM kutokana na madhila yanayoaendelea, ndio maana tunaiomba Tume iingilie kati," amesema.

“Balozi wa CCM na mawakala wanawauliza watu unatoka wapi? Balozi wa CCM ni kiongozi wa chama kwa nini wanafuatilia wananchi?" Amehoji.