Advertisement

Chadema yataka NEC ihakikishe mawakala waliokosa kiapo wanaapa

Wednesday October 21 2020
necpic

katibu mkuu wa Chadema, John mnyika

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuhakikisha kabla ya Oktoba 28 inatoa fursa ya kuwaapisha mawakala ambao hawakuapishwa leo Jumatano.

Aidha, Chadema imeitaka NEC kufanya kuwapa nakala za kiapo mawakala baada ya kuapishwa ili kuepusha kujitokeza kwa matatizo kama yaliyowahi kuathiri chaguzi zilizopita.

Kauli hiyo imekuja baada ya kazi ya kuapisha mawakala jana kukumbwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na baadhi yao kushindwa kufika sehemu za kuapia, jambo lililofanya NEC iongeze muda hadi Ijumaa.

Akizungumza na wanahabari leo Oktoba 21, ikiwa ni siku saba kabla ya wananchi kupiga kura Oktoba 28, katibu mkuu wa Chadema, John mnyika amesema NEC imeweka utaratibu kwa mawakala kuapishwa kwa msimamizi au kwa msimamizi msaidizi.

"Kuelekea Oktoba 28, siku zilizobaki tume ihakikishe inatoa fursa kwa mawakala ambao hawajaapishwa kuapa, na mwenyekiti wa NEC ajitokeze kutoa ufafanuzi wa mawakala ambao hawajaapishwa," alisema Mnyika

Alisema mabadiliko yaliyofanywa ya kuwaapisha mawakala katika ngazi za halmashauri badala ya kata, yameanza kuonyesha athari, ikiwa ni pamoja na baadhi yao kupata ajali na wengine kushindwa kwenda kuapishwa kutokana na jografia ya maeneao hayo.

Advertisement

Mnyika pia amelitaka NEC kutoa maelekezo kwa wasimamizi wa uchaguzi ili vyama vikabidhiwe nakala za viapo vya mawakala kama kithibitisho siku ya kupiga kura.

"Fomu namba sita kubaki kwa msimamizi wa uchaguzi ni tatizo kuelekea siku ya kupiga kura. Tunaitaka NEC kuwelekeza wasimamizi kutoa nakala za viapo ili mambo haya yasikirudie kama yalivyotokea katika uchaguzi mdogo wa marudio katika jimbo la Kinondonim" alisema.

"Katika baadhi ya chaguzi, hasa za marudio, tumeshuudia mawakala wakienda katika vituo na kukuta majina yao hayajabandikwa."

Advertisement