Chadema yateua makatibu sita wa kanda, nne zawekwa kiporo

Muktasari:

Kikao cha Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania kilichokutana Februari 15 na 16, 2020 jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe kimefanya uteuzi wa makatibu sita kati ya kumi wa kanda za chama hicho.

Dar es Salaam. Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema kimefanya uteuzi wa makatibu wa kanda sita kati ya kumi za chama hicho.

Uteuzi huo umefanywa hivi karibuni na kikao cha kamati kuu kilichofanyika jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini humo, Freeman Mbowe.

Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Februari 22, 2020 na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumain Makene imewataja walioteuliwa na kanda zao kwenye mabano ni; Amani Golugwa (Kaskazini), General Kaduma (Kusini) na Ali Hemed (Pwani).

Makatibu wengine walioteuliwa ni; Emmanuel Masonga (Nyasa), Gwamaka Mbughi (Kati) na Kangeta Kangeta (Magharibi).

Taarifa hiyo imesema kuwa uteuzi wa makatibu wakuu wengine wa kanda nne ambazo ni Serengeti, Pemba, Unguja na Victoria utafanyika badaye.

“Kwa upande wa kanda zingine ambazo ni Serengeti, Pemba, Unguja na Viktoria, uteuzi wa makatibu kanda hizo utafanywa na Kamati Kuu katika hatua za baadaye” amesema Makene huku waliokuwa makatibu wa kanda hizo waliomaliza muda wao watapangiwa kazi nyingine

Taarifa hiyo imeeleza kuwa uteuzi huo uliofanyika kwa mujibu wa Katiba ya Chama ya Mwaka 2006, Toleo la Mwaka 2019, ibara ya 7.7.16(c), unaanza Februari 22, 2020.