VIDEO: Msanii Harmonize azindua mgahawa wa KondeBoy, kugawa vyakula miezi sita

Sunday October 20 2019

 

Dar es Salaam. Shughuli ya ugawaji chakula iliyofanywa na msanii Abdul Rajab maarufu Harmonize imegubikwa na vurugu baada ya kutokuwepo kwa ulinzi wa kutosha.

Shughuli hiyo imefanyika leo Jumapili Oktoba 20, 2019  nje ya uwanja wa mpira

wa miguu wa Karume jijini Dar es Salam Tanzania, kupitia mgahawa wa 'KondeBoy', mradi ambao utafanyika kwa miezi sita.

Ugawaji huo ulioanza saa 7:45 na kumalizika saa 8:30 baada ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema kukata utepe na Harmonize kuanza kugawa chakula hicho kilichokuwa kimefungashwa katika mifuko midogo iliyoandikwa 'KondeBoy mgahawa'.

Watu waliokuwapo katika eneo hilo, walilizonga gari lililokuwa limebeba vyakula huku wakisukumana na kusababisha baadhi ya watu hasa watoto kudondoka chini na kukanyagwa.

Kutokana na vurugu hizo, Mkuu huyo wa Wilaya, alilazimika kuomba Polisi wachache waliokuwepo eneo hili wawatulize watu hao na wawapange kwenye mistari.

Advertisement

Baada ya Polisi kuingia wakishirikiana na walinzi wa Harmonize, hali ikatulia na watu waliendelea kugawiwa chakula hicho kwa kufuata utaratibu.

Hata hivyo, baadhi ya watu waliofika hapo akiwemo Ibrahim Salim, amesema kinachoonekana uongozi wa Harmonize haukujipanga ndiyo maana vurugu hizo zimetokea.

Hata hivyo, alipoulizwa na Mwananchi kuhusu hali hiyo, Harmonize amesema walijipanga ndiyo maana vurugu hizo zimedhibitiwa haraka.

Amesema gari hilo litakuwa likigawa chakula kila Jumapili na kadri watakavyopata wadhamini, muda wa ugawaji unaweza kuongezeka.

 

Advertisement