Changamoto za elimu zakutanisha wadau Tarime

Sunday February 23 2020

By Beldina Nyakeke Mwananchi

Musoma. Wadau wa Elimu mkoani Mara wamekutana leo Jumapili Februari 23, 2020 kujadili changamoto zinazokabili sekta hiyo ya elimu mkoani Mara hali inayopelekea mkoa wa Mara kufanya vibaya katika matokeo ya mitihani ya kitaifa kwa zaidi ya miaka mitatu mfululizo.

Akizungumza katika kongamano hilo, Mbunge wa Musoma vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo amesema kuwa anaamini kuwa kongamano hilo litakuja na suluhisho la kudumu juu ya hali ya taaluma mkoani Mara.

Profesa Muhongo amesema kuwa  inasikitisha kuona kuwa mkoa ambao ulikuwa ukifanya vizuri na kutoa wanafunzi wanaoongoza katika mitihani hiyo umekuwa ni mkoa unaofanya vibaya zaidi jambo ambalo amesema kuwa linahitaji juhudi za pamoja ili kupata suluhisho la kudumu.

“Enzi zetu tukiwa tunasoma mkoa wa Mara ulikuwa ukiheshimika sana katika sekta ya elimu lakini ghafla hali imebadilika sasa sisi kama wadau wa elimu tumeona hili sio jambo jema ni lazima kitu kifanyike ili kunusuru mkoa wetu,” amesema Profesa muhongo.

Amewataka washiriki wa kongamano hilo kushiriki kikamilifu huku akisema kuwa wadau hao wanapaswa kujadili na kuja na mapendekezo namna ya kuboresha elimu mkoani Mara.

Amesema kuwa hakuna  haja ya kulaumiana na badala yake kila mtu aone ana wajibu wa kufanya katika kuinua na kuboresha elimu mkoani Mara.

Advertisement

Akifungua kongamano hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima  amesema maazimio ya kongamano hilo yatatekelezwa na serikali ya mkoa kwa kushirikiana na serikali kuu.

Amesema kuwa sekta ya elimu mkoani Mara inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinapaswa kusemwa kwa uwazi ili ziweze kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Amesema miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na wizi wa mitihani jambo  ambalo amesema kuwa lilikuwa likifanywa na wadau mbalimbali wakiweko viongozi wa serikali, wazazi na wanafunzi wenyewe.

“Machi 2018, ofisa elimu mkoa alikuja ofisini kwangu huku akiwa amenyong'onyea sana akaniambia kuwa mkoa wetu ndio unaoongoza kwa wizi wa mitihani Tanzania nzima, ilibidi tuweke mtego na Oktoba mwaka huo tulifanikiwa kudhibiti wizi huo na mwaka uliofuata ghafla mkoa ukashuka na matokeo wote tuliyashuhudi,” amesema Malima

Advertisement