Chauma wajitoa uchaguzi Serikali za mitaa

Saturday November 9 2019

 

By Aurea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Sasa ni Chauma. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya chama cha Ukombozi wa Umma nacho kutangaza kutoshiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019.

Kimetangaza uamuzi huo siku mbili baada ya Chadema na ACT-Wazalendo navyo kutangaza kutoshiriki uchaguzi huo.

Mwenyekiti wa chama hicho, Hashim Rungwe ametangaza uamuzi huo leo Jumamosi Novemba 9, 2019 akibainisha kuwa wagombea zaidi ya 250 wa chama hicho wameenguliwa bila sababu za msingi.

“Haiwezekani nchi nzima wanaokosea kujaza fomu ni watu wa upinzani tu,  na sisi tumeamua kuwa hatutashiriki uchaguzi huu.”

“Tunaomba wagombea wetu nchi nzima wasishiriki na wao watajua wenyewe mambo ya kupiga kura huko mbele kama wataenda kupiga kura au wasiende kupiga watajua wenyewe,” amesema Rungwe.

Ameongeza, “Japokuwa tunajua hadi hivi sasa hata wanachama wetu hawana watu watakao wapigia kura kwa sababu wagombea wao wote wameenguliwa.”

Advertisement

Rungwe alitumia nafasi hiyo kuwataka wanachama wake kutulia na kuachana na masuala ya uchaguzi.

 “Kwa sababu wameshaondolewa wanafanya nini waache tena kufuatilia suala hili kwa sababu kukata rufaa tumekata rufaa lakini haisaidii chochote, uchaguzi una hila hivyo tunaungana na wenzetu kujitoa.”

Amesema haki ya kupiga kura na kugombea ni ya kila mwananchi lakini ikiwa tayari kuna watu wamewekwa kwa ajili ya kuondoa watu fulani kunaondoa maana ya uchaguzi.

 

Advertisement