China yafungua ‘mwaka wa Panya’

Dar es Salaam. Je unajua panya ana thamani gani katika maisha ya Wachina kwa mwaka 2020? Usiku wa kuamkia jana, mamia ya raia wa China waishio hapa nchini walifurika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIC), ikiwa ni shamrashamra za kufungua mwaka wao mpya.

Mwaka mpya wa Kichina utakaoadhimishwa saa 6:00 usiku Januari 25, umepewa jina la ‘Mwaka wa Panya’, ukiwa umebeba tafsiri na ujumbe katika maisha ya wachina duniani kote katika mwaka 2020.

“Tunakaribia kuanza mwaka wa panya, katika wanyama 12 nchini China, panya huashiria akili, ustadi na uboreshaji binafsi katika mambo magumu,” alisema Balozi wa China nchini Tanzania, Wang Ke katika tukio hilo ikiwa ni siku tatu tangu kuanza maandalizi ya kuelekea kilele cha sherehe hizo.

Wanyama ambao hutumika katika kuadhimisha miaka ya wachina ni pamoja na nyoka, mbwa, paka, ng’ombe, sungura na nguruwe wakibeba ujumbe kwa mwaka husika.

Katika ufafanuzi wake, balozi Wang alitumia nafasi hiyo kutuma salamu zenye ujumbe wa matumaini ya mwaka wa panya katika kuliombea taifa la Tanzania kufikia malengo ya ukuaji uchumi na uboreshaji wa maisha ya watu.

Mmoja kati ya maofisa wa Ubalozi wa China nchini Tanzania, Mganja Suleiman alisema China ndiyo taifa pekee linaloadhimisha mwaka mpya kwa kufuata mzunguko wa kalenda ya mwezi (lunar calendar) kwa karne zote katika mfumo wa maisha ya watu wa China.

Ni tukio kubwa la kitamaduni linaloadhimishwa na Wachina kote duniani, wengi hurejea nchini kwao kusherehekea kitamaduni ikiwamo kushiriki tukio la kumshuhudia mnyama aina ya dragon anayetema moto ikiwa ni ishara ya kufukuza mikosi yote iliyotokea mwaka uliopita. “Hili ni tukio kubwa sana nchini kwetu, tunaaga mwaka 2019 na kuingia mwaka 2020. Mie lazima nitakwenda nyumbani (China),” alisema Tony Lu Zang, mmoja kati ya raia wa Kichina waliojitokeza.

Sherehe hizo zilizotawaliwa na nyuso za bashasha, ziligonga nyoyo za washiriki kupitia burudani ya ngoma, michezo ya katuni ya mnyama aina ya dragon na nyimbo za kichina, zilianza saa 12:30 jioni hadi saa 4:00 usiku.

Vazi la tukio hilo lilikuwa ni rangi nyekundu ikiwa na tafsiri ya upendo.

Tanzania na China

Wakati wa sherehe hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) George Simbachawene alisema mwaka huo uwe mwaka wa kutafakari mchango walioutoa China hapa nchini, akidai urafiki wa nchi hizo umekomaa kisiasa, kiuchumi na kijamii.

“Ningependa uwe mwaka wa kutathmini 2019, niwatakie kheri na mafanikio mema katika mwaka huu mpya na muhimu kwa Wachina wote waishio hapa nchini, ni mwaka wa panya, naamini panya ni mnyama mjanja sana kwa hiyo utakuwa ni mwaka mzuri,” alisema Simbachawene.

Simbachawene aliyemwakilisha Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alisema urafiki wa nchi hizo umekomaa katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa akitamani mafanikio ya taifa hilo linaloondoa watu wake milioni 700 katika hali ya umaskini kila mwaka.

Katika hatua nyingine, Balozi Wang alisema ushirikiano kati ya Tanzania na China umeendelea kuimarika, akidai ushirikiano huo wa kiuchumi umeleta mafanikio kupitia biashara na shughuli za uwekezaji.

“Wakati huo huo ubadilishanaji wa watu na watu kati ya nchi hizi unazidi kuimarishwa katika elimu na ushirikiano pia umeendelea kupanuka. China imeipatia Tanzania ufadhili wa masomo kwa kutoa nafasi takriban 2,000 hadi sasa na zaidi ya fursa 6,000 za mafunzo ya ufundi nchini China,” alisema Wang Ke.

Alisema lugha ya Kiswahili inathaminiwa zaidi na vijana nchini China, hususani wafanyakazi wa makampuni hatua iliyochagiza kuanzishwa kwa kozi ya lugha hiyo katika vyuo vinne nchini humo. “Lakini kuna wanafunzi 10 wa China huja Tanzania kusoma Kiswahili kila mwaka katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.