Corona na anguko la uchumi wa dunia

Bila shaka na kwa kuangalia na kuzingatia misingi ya uendeshaji wa masuala ya kimataifa toka enzi na enzi, kila baada ya janga kubwa lililowahi kuitikisa dunia, kulifuatiwa na janga kubwa la kiuchumi ambalo liliitikisa dunia.

Hii ni kwa sababu, majanga makubwa yaliyowahi kuitikisa dunia yalizifanya serikali zote zitumie fedha nyingi kudhibiti athari za majanga husika na kujikuta zikiwekeza fedha kidogo kwenye masuala mengine ya uzalishaji uchumi. Hii ina maana kuwa serikali hujikuta zinatumia fedha nyingi zaidi kuliko kuingiza.

Vivyo hivyo kwa wananchi wa kawaida, hawa huwa waathirika wakubwa kwa sababu wao ndiyo wazalishaji kwenye mataifa yao. Majanga makubwa huwafanya wapunguze uzalishaji, kubaki nyumbani na kutofanya kazi au kuhofia kwenda kazini ili kulinda usalama wao na wa familia zao, matokeo yake huwa ni kuzorota au kufa kwa uchumi wa familia moja moja na hata kuyeyuka kwa mitaji ya familia husika. Majanga makubwa yanapopita huziacha nchi nyingi zikijikongoja kiuchumi na jambo hili ni la kiasili zaidi.

Vita za dunia, Vita ya Uganda

Mathalani, vita zote tunazozijua duniani ziliziacha nchi zilizohusika na vita husika au marafiki zake kwenye hali ngumu ya kiuchumi. Vita ya kwanza ya dunia iliziacha nchi zote zilizokuwa washiriki wakuu wa vita hizo katika uchumi mbovu kuwahi kutokea. Vita ya pili ya dunia ilipomalizika mataifa yaliyokuwa yanatamba duniani kama Uingereza yalipitwa na Marekani kiuchumi kwa sababu wakati Uingereza ilikuwa inapigana vita moja kwa moja, Marekani ilikuwa muuzaji mkubwa wa silaha na huduma nyingine kwenye vita hiyo, matokeo yake uchumi wa Marekani ukaimarika mno, uchumi wa Uingereza na washirika wake ukaanguka.

Nduli Idd Amin Dada alipoivamia Tanzania, ililipasa taifa letu lijilinde kwa kupeleka vikosi mpakani, baadaye Nduli alipozidisha chokochoko na dharau ikabidi Amiri Jeshi Mkuu wa wakati huo Mwl Nyerere aamuru Nduli apigwe. Vita ile ilipokwisha na Tanzania kumtokomeza Nduli, uchumi wa taifa letu uliyumba sana, uchumi wa Uganda ndiyo ulikuwa taabani mara kumi kutushinda sisi.

Kwa hakika, kila janga linapotokea na kutushambulia, lazima kutafuata kipindi kigumu cha uchumi ambacho serikali zilizoathiriwa pamoja na watu binafsi hukubali kujenga upya uchumi wake ili kurejesha matumaini ya watu wake.

Marekani na corona

Kitaalamu vikipewa jina la COVID-19, tangu vigunduliwe rasmi katika mji wa Wuhan nchini China mwishoni mwa mwaka 2019 na baadaye kusambaa duniani kote vimeweza kusambaratisha mifumo ya uchumi wa dunia, nchi moja moja, familia na watu binafsi na vimefanikiwa hasa.

Taifa la Marekani ambalo lina utajiri mkubwa sana, limetumia dola za kimarekani trilioni 2 sawa na trilioni 4,400 za kitanzania ili kuanzisha mfuko maalum wa kusisimua uchumi wa wananchi. Fedha hizo zitatumiwa kugawiwa kwa wananchi kutokana na vigezo mbalimbali na hazihusiani kabisa na oparesheni zingine zozote za kupambana na ugonjwa wa corona nchini humo.

Inasadikiwa kuwa hadi Marekani inafanikiwa kupambana na ugonjwa huo itagharamika kiasi cha dola za Kimarekani zipatazo trilioni 6 sawa na shilingi za kitanzania trilioni 13,200. Fedha hizo ni sawa na bajeti za miaka zaidi ya 300 za nchi zote zilizoko Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara. Lakini Marekani inapaswa kuingiza pesa hizi kwenye corona, virusi ambavyo vimeivamia na vinaishambulia dunia bila huruma.

Dunia nzima inaathirika

Wakati Marekani inatumia utajiri wote huo kuwekeza kwenye mapambano dhidi ya corona, nchi nyingine duniani zimeumizwa ipasavyo. China ambayo haihitaji sana takwimu zake za kuumizwa kiuchumi, imetumia nguvu ya ziada kutuliza hali ya kutisha ya madhara ya virusi vya corona. Italia ambayo raia wake wameangamia sana imetumia zaidi ya dola trilioni 1 kupambana na maambukizi ya virusi vya corona na hadi sasa mapambano yanaendelea na pesa nyingi zinatumika.

Nchi nyingi kwenye mabara yote zimetangaza sera au amri za kukaa ndani au kutembea kwa vibali maalum na shida maalum sana. Mfumo mzima wa maisha ya wananchi ambayo yaliwarahisishia kupanga masuala ya kiuchumi, umevurugika na haufai tena.

Viwanda muhimu kwenye nchi zenye tishio kubwa la virusi vimefungwa na biashara za kati na ndogo zimefungwa pia. Hata nchi ambazo bado zinaendelea kuzalisha bidhaa mbalimbali, ununuliwaji wa bidhaa hizo umeshuka mno, familia moja moja zimeanza nidhamu ya matumizi ya fedha kwa sababu hawajui kesho nini kitatokea.

Tutumie akili zaidi

Dunia inapoingia kwenye majanga makubwa kama haya, suala la kujilinda na kuzilinda familia zetu ni la kila mmoja wetu. Serikali zinajitahidi sana kutoa elimu na tahadhari zote muhimu za kujikinga na corona, lakini ni jukumu la kila mtu mmoja mmoja, yeye na familia yake kuzingatia tahadhari hizo.

Ni muhimu zaidi kwamba wakati huu kila familia ilinde uchumi wake, kila familia ijue kuwa kuna anguko la uchumi kwa dunia nzima linakuja na anguko hilo linakuwa baya zaidi ikiwa familia zitakuwa hazijajipanga kulikabili. Ni muhimu kuweka msisitizo kuwa serikali zote duniani huja na mipango ya jumla ya kukabiliana na anguko la uchumi na mambo mengine yote yanayohusu kujizatiti kwa kina na kwa ziada hufanywa na mtu mmoja mmoja kwenye familia yake.

Wakati huu ambapo corona inapamba moto na kufyonza uchumi wote wa dunia ni muhimu kila familia zikaweka nidhamu za matumizi ya fedha na kuondoa masuala yote ambayo siyo ya lazima. Miundombinu ya familia na matumizi yake vielekezwe kwenye kutunza chakula na fedha za akiba, usalama wa familia na kujikinga na korona huu siyo wakati wa matumizi na matanuzi.

Hakuna vikao vya maelekezo

Kwa kawaida, huwa hakuna vikao vya maelekezo kwenda kwa wananchi mbalimbali kuwalazimisha namna ya kutumia fedha na akiba zao, tunafahamu kuwa hili ni jambo binafsi sana. Mathalani, muda huu ukitumia fedha zako vibaya na baadaye kukawa hakuna biashara nzuri kwenye duka lako, utakosa chakula ndani. Chakula kikikosekana kama serikali italeta msaada wa chakula hautaleta kwa familia moja moja tu, utaziletea zote ambazo zimeathirika sana.