Corona yapangua utaratibu wa misa Alhamisi, Ijumaa Kuu

Wahudumu wa kanisa la Full gospel Bible fellowship wakiwapima  joto la mwili waumini wa kanisa hilo kabla ya kuingia ndani ya kanisa hilo kwa ajili ya ibada ya jumapili ya matawi  jijini Dar es Salaam jana. Picha na Ericky Boniphace

Dar es Salaam. Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam limebadili utaratibu wa uendeshaji wa misa za Alhamisi Kuu na Ijumaa Kuu likiondoa matukio ya kunawishana miguu na kubusu msalaba.

Utaratibu kama huo, ambao unalenga kuepuka maambuziki ya ugonjwa wa virusi vya corona, Covid-19, pia umetangazwa na Kanisa Katoliki.

Padri Jerome Napela wa Parishi ya Mtakatifu Nikolao na Mashahidi wa Afrika, amesema katika misa ya Alhamisi Kuu Aprili 9, hakutakuwa na kutawazwa miguu kwa wazee 12 kama ilivyo kawaida.

Padri Napela alisema huo ni mwongozo na maelekezo yaliyotolewa Aprili 2 na uongozi wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam.

“Ibada ya Ijumaa Kuu tulikuwa na utaratibu wa waumini kuubusu msalaba, lakini mwaka huu waumini watalazimika kuuinamia.

“Tukio la wazee kutawazwa halina mbadala wake wa kuliadhimisha,” alisema Padri Napela.

Padri huyo ametoa wito kwa waumini kufuata kile kilichoagizwa na Serikali kuhusu kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona badala ya kufuata yale yanayoenezwa mitandaoni.

Alisisitiza kuwa msemaji wa masuala hayo ni viongozi wa juu waliotangazwa na si mitandao ya kijamiii.

“Hata mimi sina mamlaka ya kuuzungumzia ugonjwa wa corona, lakini nina haki ya kuzungumzia afya ya kiroho,” alisema.

“Achaneni na habari za mitandaoni, fuateni maelekezo ya Serikali na wakuu wa nchi. Tukiambiwa na makondakta gari ni level seat tutii,” alisema Napela.

Alisema kanisa hilo linaendelea kumuomba Mungu ili aiepushe nchi na madhara makubwa ya ugonjwa huo ambao umeshaua zaidi ya watu 64,800 kote duniani hadi jana mchana.

Katibu wa kanisa hilo, Johnn Kibata alisisitiza waumini kunawa na kupaka vitakasa mikono.