DC, DED Nachingwea matatani…Rais atoa onyo

Muktasari:

  • Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Nachingwea Bakari B Bakari  na Mkuu wa wilaya hiyo Rukia Muwango wameingia matatani baada ya wananchi kuwachongea kwa Rais wa Tanzania John Magufuli chanzo kikiwa ni ucheleweshaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo soko na stendi wilayani humo.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania John Magufuli amewabana Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea (DC) Rukia Muwango na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Bakari B Bakari baada ya wananchi kulalamikia ucheleweshwaji wa miradi ya maendeleo.

Tukio hilo limetokea leo Jumatano Oktoba 16, 2019 wakati Rais akihutubia wananchi katika wilaya ya Nachingwea ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika mkoa wa Lindi.

Baada ya hotuba za viongozi mbalimbali, Rais alimuomba Mwenyekiti wa CCM, Mzee Hashim Mkanjauka aeleze matatizo yote yanayowakabili wakazi wa Nachingwea.

Mkanjauka alianza kuelezea miradi ya maendeleo iliyokwama hali iliyowafanya wananchi waibuke kwa shangwe na hivyo kumfanya Rais atake kujua Zaidi kero hizo.

“Viongozi wetu siyo wakweli, miradi wilaya ya Nachingwea vijijini haitekelezeki, stendi ya wajasiriamali hakuna, soko halina kitu mkandarasi waliyempa hajamaliza, redio imenunuliwa na kufungwa kwa fedha za wananchi zaidi ya Sh100 milioni lakini haifanyi kazi. Maji yamekuja na mwenge yameondoka na mwenge Nachingwea ni wilaya kongwe,” amesema Mzee Mkanjauka.

Baada ya maelezo hayo Rais alimuita Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo akimtaka atoe majibu ya kwanini miradi hiyo inasuasua na mingine imesimama kabisa.

“Sh200 milioni ilijenga sehemu ya kupumzikia wasafiri , mabanda 12 ya biashara sisi tulikuta imefungwa tuliwekeza kwa kuweka mabanda kwa mapato ya ndani ya Sh81 milioni, kujenga mabanda 26 kumalizia choo na kuanza kwa kuwa ni kubwa maeneo tuliyotenga kwa ajili ya wajasiriamali itabidi tuyapimie wameshapimiwa na wanaohitaji miundombinu ni mama lishe.”

Majibu hayo yalizalisha maswali zaidi kwamba ni kiasi gani hasa kilichotumika kwa upande wa soko pekee, Mkurugenzi huyo alijibu kuwa ni Sh71 milioni.

Baadaye Rais aliamua kushuka katika gari na kutembea mita kadhaa eneo la soko ili kujiridhisha kama kweli ujenzi unaendana na thamani ya fedha inayotajwa.

Baada ya kufika katika soko hilo na kuona hali halisi, alitaka kujua Sh71 milioni namna zilivyotumika lakini Mkurugenzi alionekana kujikanyaga namna alivyokuwa anajibu.

Ashura Ally mmoja kati ya wananchi aliulizwa changamoto ya soko hilo na mbele ya Mkurugenzi huyo alijibu, “Ujenzi huu ulianza tangu mwaka jana Novemba sisi wafanyabiashara hapa tulihamishiwa soko jingine na mpaka leo tumeshatimiza mwaka kinachofanyika hakieleweki.”

Baada ya hapo Rais aliondoka eneo la soko na kwenda katika eneo la stendi lililopo mita chache kutoka eneo hilo. Alianza kumuuliza tena Mkurugenzi huyo kwanini aliwahamisha wakati stendi haijakamilika?

Mkurugenzi alijibu; “Nilipewa maagizo kutoka kwa mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya.”

Rais alimuita Mkuu wa Mkoa ili ajibu swlai hilo;

RC: “Nilikuja nikatembelea stendi na soko mazingira niliyoyakuta hayakuniridhisha, nikawaambia mfanye marekebisho niliagiza halmashauri watenge eneo la muda kupisha ukarabati tatizo ikawa ni kasi ndogo.”

Rais Magufuli: Kwanini soko halikuisha kwa mwaka mzima?

RC: Tulipokea maelezo kuwa mapato hayatoshi.

Rais: Mkurugenzi mnapokea Sh ngapi kuutoka Hazina?

Mkurugenzi: Tunapokea Sh27 bilioni kutoka wizara ya fedha.

Rais: Mnazitumia vipi? Kulikuwa na shida gani? Hizo fedha mnazipeleka wapi wakati zimeletwa kwa ajili ya maendeleo?

Mkurugenzi:  Sehemu ya mishahara tunatumia kama Sh17 bilioni na fedha zingine zinaendesha Halmashauri

Rais: Asilimia 40 lazima zitumike kwenye ukarabati wa soko na fedha za ndani, zinatumika wapi? Kwanini zilizotoka hazina hamjazitumia hapa?

Mkurugenzi: Sh400 tulizitumia katika ujenzi wa wodi ya wazazi hospitali ya wilaya.

Rais: Naibu Waziri njoo hapa utuambie fedha za ukarabati wa wodi ilitoka wapi?

Dk Ndugulile: Zilitoka serikali kuu.

Baada ya hapo Rais alionyesha kutokufurahia majibu ya Mkurugenzi huyo na aliwaomba wananchi kuwa wavumilivu ili aweze kurekebisha suala hilo, “Nitapata majibu haraka iwezekanavyo.”

Alipofika kijiji cha Shewende Rais alitoa onyo kwa DED na DC huyo kuhakikisha wanarekebisha kasoro alizokutana nazo.

“Dc na mkurugenzi wabadilishe tabia zao fedha zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo zitumike na watu wazione. Zimetengwa Sh27 bilioni mmezifanyia nini? Hapa ameniudhi kweli Mkurugenzi wenu,  na DC uwe mkali wewe ndiyo mwenyekiti wa ulinzi na usalama wa kamati hii, wakati na mkuu wa mkoa unapotoa maagizo lazima ufuatilie yanatekelezwaje.

“Kwa sababu kero tuliyoikuta pale Nachingwea haikutakiwa wananchi walalamike, Mkurugenzi  anajifanya amekaa marekani inaudhi sana mnatakiwa hizi fedha zinazotolewa na Serikali zikafanye kazi,” amesema Rais.