DC Chemba aiomba mahakama kutoa Sh50,000 za chakula kila mwezi kwa ajili ya mwanaye

Tuesday August 20 2019

 

By Tausi Ally, Mwananchi [email protected] mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Chemba  mkoani Dodoma nchini Tanzania, Simon Odunga ameiomba Mahakama ya Mwanzo Ukonga kumruhusu awe anatoa Sh50,000 kila mwezi kwa ajili ya mwanaye kununuliwa chakula.

Odunga aliyefungua kesi kuwataliki wake zake wawili mahakamani hapo alitoa kauli hiyo katika kesi ya madai ya talaka namba 180 ya mwaka 2019.

Mtoto huyo mwenye umri wa miaka minne ni aliyezaa na mkewe mdogo, Ruth Osoro.

Jana Jumatatu Agosti 19, 2019,  Mediliana Mbuwuli ambaye  ana ndoa ya Kikristo na Odunga aliiomba mahakama isivunje ndoa ya mkemwenza, bali isimamie atunze familia yake.

Medilina alikuwa shahidi katika kesi iliyofunguliwa na mkuu huyo wa wilaya kutaka mahakama imruhusu kumtaliki Ruth.

Katika maelezo yake mahakamani hapo, Odunga amesema atatoa kiasi hicho cha fedha kila mwezi ikiwa mahakama itaamuru mtoto huyo aishi na mama yake.

Advertisement

Kuhusu matibabu ya mwanaye, amesema mtoto huyo ana bima ya afya na kwamba atamlipia ada ya shule kadri itakavyokuwa.

Baada ya maelezo hayo, Ruth alipinga kuwa Sh50,000 ni ndogo na haiwezi kukidhi mahitaji.

Ruth aliiomba mahakama hiyo imuamuru mkuu huyo wa wilaya kupeleka risiti ya mshahara wake ili kujua kiwango kitakachokidhi mahitaji.

Hakimu Elia Mrema alimtaka Ruth kupendekeza kiwango anachoona kinakidhi mahitaji hayo, mwanamke huyo kutaka awe anapatiwa Sh1 milioni.

Odunga alipinga kiasi hicho cha fedha kwamba ni kikubwa ikilinganishwa na kipato chake, kwamba Sh50,000 ni sahihi kutoa kwa kuwa ana watoto wengine watatu.

Mkuu huyo wa wilaya amesema analipwa Sh2.7 milioni na akikatwa pamoja na mikopo anayodaiwa anabaki na Sh1 milioni hivyo hawezi kutoa kiwango kilichopendekezwa na Ruth.

Amesema mahakama katika uamuzi wake wa Agosti 23, 2019 iamuru apatiwe mwanaye amlee na ikishindikana awe huru kumtembelea.

Hakimu Mrema amesema mahakama itatoa uamuzi Agosti 23, 2019.

 


Advertisement