DC Kinondoni aunda kamati kuchunguza Hoteli ya Coco Beach iliyoteketea

Muktasari:

Hoteli ya Coco Beach iliyopo Dar es Salaam imetekelea leo Jumapili na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo ameunda kamati ya kuchunguza chanzo cha moto huo ambapo ameipa siku tatu kukamilisha uchunguzi huo.

Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni (DC) mkoani Dar es Salaam nchini Tanzania, Daniel Chongolo ameunda kamati ya watu sita kuchunguza tukio la ajali ya moto uliotekeleza Hoteli ya Coco Beach.

Hoteli hiyo iliyopo imeanza kuteketea kwa moto kuanzia saa 7:30 mchana wa leo Jumapili Septemba 22, 2019 ambapo Mmiliki wa hoteli hiyo, Alphonce Buhatwa ameiambia Mwananchi kuwa asilimia 80 ya mali zote katika hotel hiyo zimeteketea.

Akizungumza na Mwananchi leo usiku Jumapili, DC Chongolo amesema, “nimekwenda hapo jioni ya saa moja na nimeunda kamati ya watu sita itakayofanya kazi kwa siku tatu kuanzia leo na Jumatano mchana wataikabidhi taarifa kwa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa.”

Chongolo amewataja wajumbe wa kamati hiyo itakayoongozwa na polisi ni Jeshi la Zima Moto na Uokoaji ambao katika kamati hiyo watakuwa ni katibu pamoja na wajumbe kutoka usalama wa taifa, mwanasheria na mtaalamu kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Amesema kikubwa itakachokifanya ni kuchunguza chanzo cha moto huo.