DC Morogoro aagiza wazazi kuwachapa viboko watoto wao

Baadhi ya Wanafunzi waliohusika na kuandika Matusi na kuchorachora kwenye kuta za madarasa na vyoo vya shule ya Sekondari Mjimpya manispaa ya Morogoro wakichapwa viboko na wazazi wao

Muktasari:

Wanafunzi 11 wa Shule ya Sekondari Mjimpya iliyopo manispaa ya Morogoro wameadhibiwa viboko vitano kila mmoja na wazazi wao baada ya kutuhumiwa kuchora majengo ya shule hiyo.

Morogoro. Mkuu wa wilaya (DC) ya Morogoro nchini Tanzania, Regina Chonjo ameamuru wazazi kuwachapa viboko vitano wanafunzi wa kidato cha tatu na nne kila mmoja waliohusika na uharibifu wa baadhi ya majengo ya shule ya sekondari Mjimpya iliyopo manispaa ya Morogoro.

Wanafunzi 11 wa shule hiyo wanadaiwa kufanya uharibifu huo kwa kuchora chora na kuandika matusi mbalimbali kwenye kuta za majengo hayo. Adhabu hiyo ilitolewa mbele ya wazazi wenyewe na wanafunzi wenzao.

Mkuu huyo wa wilaya aliamua kutolewa kwa adhabu hiyo baada ya Novemba 8, 2019 kufika katika shule hiyo kuangalia uharibifu huo.

Leo Ijumaa Novemba 15, 2019, Chonjo amesema ujenzi wa madarasa hayo mapya ulifuatiwa ya awali kuvunjwa baada ya kupitiwa na ujenzi wa reli ya kisasa na kuamua kujengwa kwa madarasa upande mwingine.

Amesema shule hiyo imeanza miezi miwili iliyopita baada ya kukamilika kwake kwani awali wanafunzi wapatao 400 baada ya shule kuvunjwa na walihamishiwa shule jirani ya Tushikamane ili kuendelea na masomo.

Mkuu wa Shule hiyo, Zakayo John amesema wanafunzi saba ndio waliofika shuleni hapo na kupewa adhabu huku wanne wakigoma kufika na kuonekana kutotii wito wa mkuu huyo wa wilaya.

John alisema wanafunzi hao 11, nane ni wa kidato cha nne na watatu ni wa kidato cha tatu, huku akieleza kuwa walifanya uharibifu huo wakati wakiendelea na mitihani ya kidato cha nne.

"Wakati mtihani ikiendelea walikuwa wakiomba ruhusa na kwenda chooni huko ndiyo walikuwa wakiandika matusi na kuchora picha za ovyo, wengine walifanya hivyo baada ya mitihani kumalizia," alisema.