DC Nanyumbu awataka walio maeneo salama kutulia majumbani

Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara, Moses Machali

Muktasari:

  • Kuepuka taharuki kwa wananchi kufuatia taarifa za kuwapo kimbunga Keneth, wananchi wametakiwa  kutulia majumbani na walio maeneo hatarishi kuondoka

Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara, Moses Machali amewataka wananchi wilayani humo watulie majumbani ikiwa maeneo wanayoishi ni salama na wale walio katika maeneo hatarishi kuondoka mara moja.

Amesema ili kuepuka athari za kimbunga Keneth kilichotangazwa kuwa huenda kikayakumba maeneo hayo, wananchi hawapaswi kupata taharuki na kwani wametengeneza mfumo wa mawasiliano na Serikali za vijiji kupata taarifa zote muhimu kama kikitokea.

Akizungumza na Mwananchi Digital kwa njia ya simu leo, Machali amesema wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya namna ya kujikinga na kimbunga hicho.

Ametaja makundi yanayoendelea na kazi mpaka sasa katika wilaya hiyo kuwa ni watumishi wa afya katika zahanati, vituo vya afya na hospitali, huku wengine wakitakiwa kubaki majumbani wakiwamo wanafunzi.

“Pia vikosi vyote vya ulinzi na usalama kama polisi, wanajeshi wapo kazini kama kawaida na tumeandaa mtandao wa mawasiliano ya kupata taarifa popote likitokea jambo,” amesema.

Hata hivyo, mkuu huyo wa wilaya amesema hali ya hewa tangu asubihu ni tulivu, isipokuwa kua baridi na upepo kwa mbali.