DC Sabaya aagiza wamiliki wa mabasi kukamatwa kwa madai ya kuhujumu miundombinu reli Dar-Moshi hadi Arusha

Sunday January 19 2020Mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya

Mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya 

By Daniel Mjema, Mwananchi [email protected]

Moshi. Mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya ameagiza wamiliki wawili wa mabasi kukamatwa kwa tuhuma za kuunda genge la uhalifu kwa lengo la kuhujumu miundombinu ya reli ili kuathiri usafiri wa treni ya abiria kati ya Dar es Salaam- Moshi hadi Arusha.

Wafanyabiashara hao waliotakiwa kuripoti kituo cha Polisi Bomang'ombe leo Jumapili Januari 19, 2020 kabla ya saa 10 jioni ni Clemence Mbowe anayemiliki mabasi ya Machame Safari na Rodrick Uronu anayemiliki mabasi ya Lim Safari.

Sabaya ametoa kauli hiyo leo Jumapili Januari 19, 2020 katika kijiji cha Rundugai Wilaya ya Hai wakati akikagua ukarabati wa reli.

Wakati Sabaya akieleza hayo, Mbowe alipoulizwa na Mwananchi kuhusu tuhuma hizo amesema si za kweli.

Mfanyabiashara huyo amesema  hana sababu ya kuunda genge hilo kwa kuwa biashara yake ya mabasi ni kati ya Moshi, Arusha na Dar es Salaam.

Amesema yeye si mwanasiasa na kudai kuwa Sabaya anataka kuchafua majina ya watu, atatafuta haki yake mahakamani.

Advertisement

Kwa upande wake Uronu amesema, “kama tuna tuhuma angetuita ofisini maana ni kiongozi na ana ofisi kwa nini aongee katika mkutano wa hadhara kwa tuhuma ambazo hazipo.”

“Mimi sina treni ya abiria sishindani na treni, ikitokea mfanyabiashara wa mabasi ananilalamikia ningeelewa, mimi na mabasi wapi na wapi? Kuna vyombo vya haki vitapima nani mwenye haki.”

Advertisement