DC Ubungo agawa vitambulisho vya wafanyabiashara

Muktasari:

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori amegawa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo wilayani humo na kuwataka kuvitumia vyema


Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori amegawa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo wilayani humo na kuwataka kuvitumia vyema.

Amesema watakaobainika kwenda kinyume na matumizi ya vitambulisho hivyo watanyang'anywa.

Makori amegawa vitambulisho hivyo leo Jumatano Desemba 12, 2018 katika soko la Mawasiliano ya Simu -2000  wilayani humo.

Amewataka wafanyabiashara hao kutokubali kutumiwa kuuza bidhaa za wafanyabiashara wakubwa wanaodaiwa kukwepa kulipa kodi.

"Tukikubaini tunakunyang’anya kwa sababu utakuwa umekwenda kinyume na matumizi  ya vitambulisho hivi. Pia naomba  mjaze kwa usahihi  taarifa zenu kwenye fomu ya  kuomba kitambulisho," amesema Makori.

Mkuu wa wilaya huyo amesema awamu ya kwanza watatoa vitambulisho 5,000 kwa wafanyabiashara hao na vikiiisha wataongeza vingine kwa waliosalia.

Amewataka watakaopata vitambulisho hivyo kuanza kazi mara moja na watembee vifua mbele kwa sababu wana uwezo wa kufanya shughuli zao sehemu yoyote nchini.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa soko hilo, Francis Mulamula  amemshukuru Rais John Magufuli kwa kutoa vitambulisho hivyo vitakavyowasaidia kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

“Kwa nyakati tofauti tumekuwa tukifukuzwa na mamlaka husika lakini sasa hivi tumepata mkombozi wa changamoto hiyo,” amesema Mulamula.

Kwa mujibu wa Mulamula, manispaa ya Ubungo imetumia orodha ya wafanyabiashara iliyopo kwenye soko hilo katika mchakato wa kugawa vitambulisho hivyo.