DC atangaza operesheni tokomeza wanaume teleza

Monday May 27 2019

By Anthony Kayanda, Mwananchi [email protected]

Kigoma. Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Samson Anga ametangaza kiama kwa wanaume teleza wanaobaka wanawake usiku na wanaoleta ukinzani hushambuliwa na kujeruhiwa kwa vifaa vyenye ncha kali kiasi cha kuhatarisha usalama wao.

Operesheni hiyo inayoendeshwa na polisi mkoani Kigoma inahusisha misako na doria mitaa ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Hatua hiyo imekuja baada ya mkuu huyo wa wilaya kufanya ziara kata ya Mwanga Kusini ambako kumetokea vitendo vya ubakaji na watu kuumizwa kwa kukatwa mapanga na kuchomwa visu.

Anga ameanza ziara yake leo Jumatatu Mei 27, 2019 kwa kutembelea hiyo kwa ajili ya kujua changamoto zilizopo, pamoja na mambo mengine sakata la teleza limepewa kipaumbele.

"Hili suala la teleza nimelisikia sikia muda mrefu toka nimekuja (Kigoma 2016) lakini sikujua kama ni kubwa kwa kiwango mnachoeleza, watu wanazungumza kuhusu teleza kana kwamba sio jambo kubwa," amesema Anga na kuongeza:

"Wanawake mnaniomba niwasaidie hawa teleza wakamatwe, nawahakikishia huyu teleza atakoma. Kabla sijaondoka Kigoma nitahakikisha teleza wamekwisha na msingi nitakaouweka hata akija mkuu wa wilaya mwingine hatopata shida."

Advertisement

Ameahidi kwamba wanaume watakaokamatwa watafungwa gerezani ili iwe fundisho kwa wengine.

"Nataka hawa teleza wanapokamatwa wakifikishwa Polisi wapigwe fimbo nyingi sana na wanapokwenda mahakamani wafungwe, nawaambia wataozea jela," amesema Anga.

Amesema operesheni hiyo itakuwa endelevu katika Manispaa ya Kigoma Ujiji hadi teleza watakapotoweka.

Baadhi ya wanawake wamesema wanawajua wanaume teleza, lakini wanaogopa kuwataja hadharani kwa vile wanaweza kudhuriwa.

Jovina Simon anasema mwaka jana 2018, teleza alivamia nyumbani kwake akaingia chumba cha watoto wa kike na kuchana nguo ya ndani ya mmoja wa mabinti zake, lakini alipomtisha kuwa akipiga kelele atamkata panga binti huyo alimwambia haogopi kwa vile alikuwa amemtambua.

"Kesho yake mtoto wangu wa miaka tisa alimuona na kutwambia kwamba yule teleza yupo jirani na hapo nyumbani, nilipomwambia kitendo alichofanya alikataa na kututukana matusi ya kilaana," amesema Jovina.

Amesema kutokana na tukio hilo walitoa taarifa Polisi lakini wakakosa ushirikiano kiasi cha kukata tamaa kufuatilia kesi hiyo licha ya kwamba kulikuwa na ushahidi wa kutosha kwa vile watoto walimuona alivyoingia ndani akiwa uchi.

Naye Majaliwa Ally wa mtaa wa Muhongwe kata ya Mwanga Kusini, analalamika juu ya kundi la vijana kukaa jirani na nyumba yake huku wakivuta bangi.

"Nimetoa taarifa mara kadhaa kwa mwenyekiti wa mtaa lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa. Bangi ni dawa za kulevya lakini watu wanavuta ovyo, tunapata madhara kutokana na moshi wake na wanaongea matusi ya nguoni," amelalamika Ally.

Mkuu wa wilaya anaendelea na ziara yake katika kata mbalimbali ili kupata maoni na kero zinazowakabili wananchi.

Advertisement