DEMOKRASIA: Chadema na kilio cha tume huru msibani

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mboe akizungumza wakati wa  maziko ya  mzee Elias Mwingira ambae ni  Baba Mzazi wa Mtume wa Kanisa la EFATHA  Josephat Mwingira, Kibaha, Pwani jana.Picha na Mtandao

Kibaha. Viongozi wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe jana walitumia msiba wa Elias Mwingira ambaye ni baba mzazi wa kiongozi wa Kanisa la Efatha, Mtume na Nabii Josephat Mwingira kudai tume huru ya uchaguzi nchini.

Pia, wamemuomba kiongozi huyo wa dini kushirikisha viongozi wa dini wa madhehebu mbalimbali nchini kuliombea Taifa kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu.

Mbali Mbowe, viongozi wengine wa Chadema waliowasilisha kilio hicho baada ya kupewa nafasi ya kutoa salamu katika ibada ya mazishi iliyofanyika Kibaha mkoani Pwani ni katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika; mwenyekiti wa Kanda ya kati, Lazaro Nyalandu na mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la chama hicho (Bawacha), Halima Mdee.

Pia alikuwepo mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson na mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa.

Kilio cha viongozi hao kimekuja ikiwa imepita wiki moja tangu kilipofanyika kikao cha siku mbili cha kamati kuu ya chama hicho.

Baada ya kumalizika kwa kikao hicho, viongozi wa Chadema hawakueleza maazimio hadi jana walipotoa kilio chao katika msiba, huku pia ikitolewa taarifa ya uteuzi wa makatibu sita wa kanda.

Madai ya tume huru ya uchaguzi imekuwa ajenda kuu ya Chadema na vyama vingine vya upinzani nchini. Februari 3, mwaka huu Mbowe aliviambia vyombo vya habari jijini Dar es Salaam kuwa Januari 29, 2020 alimwandikia Rais John Magufuli kuomba Serikali kufanya mabadiliko ya sheria yatakayowezesha kuundwa kwa tume huru kabla ya Oktoba.

“Huu ni mwaka wa uchaguzi, kwa hali ilivyo kuna kila aina ya kiashiria cha kutokea machafuko ya kisiasa kama hatutazika viburi vyetu vya kiitikadi na kusimama pamoja,” alisema Mbowe.

Ibada ya mazishi

Ibada hiyo ilifanyika katika ukumbi wa kanisa hilo unaotumika kufanya makongamano uliopo katika eneo la kanisa lenye ukubwa wa takribani ekari 500.

Elias Mwingira alifariki dunia Januari 22, mwaka huu akiwa na umri wa miaka 94 na jana ndio yamefanyika mazishi yake huku mamia ya watu wakishiriki wakiwemo viongozi wa dini kutoka mikoa mbalimbali na nje ya nchi pamoja na wanasiasa.

Baada ya viongozi hao kuwasilisha ombi hilo, Mtume Mwingira alimtaka Mbowe na wenzake kuwa wavumilivu, “mvumilivu hula mbivu..., nimesikiliza maneno yenu ya kisiasa na kiserikali na nimeyatunza, nilichogundua mnahitaji kulelewa kiroho ili mfike mwisho wa safari msiishie njiani.”

Katika salamu zake Mbowe alimuomba Nabii Mwingira kwa kushirikiana na watumishi wengine kuliombea Taifa ili haki iweze kutawala katika uchaguzi mkuu.

Alisema baraka ya amani, upendo na mshikamano ambao Taifa limepewa na Mungu haipaswi kudharauliwa wala kupuuziwa.

“Ombi langu kwa Mtume Mwingira ukaungane na watumishi wengine kuliombea Taifa na viongozi wenye jukumu la uchaguzi kwa kuwa ndio wenye uamuzi wote,” alisema Mbowe.

Kiongozi huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni alisema mwaka huu utafanyika uchaguzi wa madiwani, wabunge na rais, ni vyema kufanyika maombi ya kuliombea Taifa.

Mbowe ambaye ni mbunge wa Hai alimwomba Mwingira kuwaombea viongozi wa kisiasa kuacha kiburi na kutambua mamlaka zilizopo zinapita lakini wanadamu wapo.

Kwa upande wake Mnyika alisema, “tunawaomba watumishi wa Mungu kuombea Taifa ili haki iweze kutamalaki. Haki huinua Taifa bali dhambi ni aibu kwa watu wote. Kupitia msiba wa mzee Mwingira mkaliombee Taifa wakati wakuelekea uchaguzi tukawe na tume itakayosimamia uchaguzi huru na wa haki.”

Naye Nyalandu alisema, “kwa baba yetu Mwingira nilimfahamu Mungu aliweka vitu fulani vya tofauti kwake. Mungu awatumie ili mrudishe amani iliyokuwepo enzi za Nyerere (Julius-rais wa kwanza wa Tanzania), akairuhusu hii nchi haki itendeke kwenye mioyo yetu.”

Dk Tulia alisema mtu hapaswi kumhukumu mwingine kulingana na jambo alilofanya kwa kuwa hata maandiko matakatifu yanaeleza na kubainisha kuwa jambo husika linaweza kuwa na faida kwa jamii.

Akitoa shukrani kwa watu waliofika msibani, Mwingira alimtaka Mbowe kuwa mvumilivu ili ale mbivu.

“Mbowe wewe umebanwa na umeminywa sana. Nimegundua jambo kwako wewe ni mvumilivu sana na mvumilivu hula mbivu, endelea kuwa mvumilivu.

“Kama wanasiasa mnatakiwa kulelewa hata baba yangu aliniambia usishindwe na mimi nawaambia wanasiasa msitangaze maneno ya kushindwa,” alisema Mwingira.

Alieleza kuwa kila aliye mwanasiasa ajue atashinda kila aliyefika kwenye msiba huo ajue ameshinda na wenye agenda ya kushindwa hawajaja.