DPP: Tutazishtaki benki zitakazokiuka sheria, masharti na taratibu za kazi

Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania (DPP), Biswalo Mganga

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania (DPP), Biswalo Mganga amesema ofisi yake haitasita kuzichukua hatua na kuzishtaki benki ambazo zitakiuka sheria na taratibu za ufanyaji kazi kwa kuwafungulia watu akaunti ambazo wanazitumia kutapeli.
Amesema hayo baada ya kuwepo kwa matukio ya watu kufungua akaunti katika benki mbalimbali na kuzitumia kutapeli watu, wafanyabiashara na taasisi binafsi.
Biswalo amesema hayo leo Alhamisi, Aprili 9, 2020, muda mchache baada ya mshtakiwa Dioniz Kaskazi kusomewa mashtaka sita yakiwemo ya kutapeli na kujipatia fedha kiasi cha Sh27 milioni kwa njia ya udanganyifu.
Akizungumza na waandishi wa habari Biswalo amesema Kaskazi alifungua akaunti katika benki ya CRDB Tawi la Msasani kwa jina la mapato ya ndani, huku akijua kuwa ni kosa kisheria.
Hata hivyo, amesema ofisi yake inaendelea na uchunguzi kubaini ofisa wa benki aliyehusika kumfungulia akaunti mshtakiwa huyo, wakati akijua kuwa akaunti yenye jina la mapato ya ndani inatumiwa na Serikali kwa ajili ya kukusanya mapato na sio mali ya mtu binafsi.
“Natoa tahadhari kwa benki pamoja na watumishi wao kwamba wasipofuata utaratibu wa kuwajua wateja wao wanaofungua akaunti basi benki hizo zitaanza kuwajibika zenyewe kwa sisi kuwashtaki," amesema Biswalo na kuongeza.
"Benki zinawajibu wa kusimamia na kuangalia watu wasiingize fedha ovyo ovyo bila kufuata utaratibu, sasa itafika hatua benki moja moja licha ya kuwachukulia hatua watumishi wake tutaanza kuzishitaki na benki zenyewe."