DPP Mganga asamehe mahabusu 150 gereza la Geita

Wednesday December 18 2019

By Emmanuel Mtengwa, Mwananchi

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) nchini Tanzania, Biswalo Mganga amesema jana Jumanne 17, 2019 amewasamehe mahabusu 150 kwenye gereza la Geita.

DPP Mganga amesema hayo leo Jumatano Desemba 18, 2019 alipoulizwa na Rais wa Tanzania, John Magufuli katika hafla ya uzinduzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya ya Chato na uwekaji wa jiwe la msingi ujenzi wa jengo la Zimamoto na Uokoaji la Wilaya ya Chato mkoani Geita.

Mkuu huyo wa nchi alikuwa anazungumzia mlundikano wa mahabusu kwenye magereza mbalimbali nchini bila kupelekwa mahakamani.

“Nimefurahi DPP yuko hapa na nafahamu hatua zinazochukuliwa na wizara ya sheria na katiba katika kutembelea magereza mbalimbali na kuangalia watu waliokaa mule bila kupelekwa mahakamani na wengine wana kesi ndogo tu” amesema Rais Magufuli

“Ninashukuru hatua mmeanza kuchukua, katika mikoa mitatu tu mliyotembelea mmeshasamehe na kuwatoa watu 601 kwa taarifa nilizonazo, si ndiyo?” alihoji Rais

“Ndio mheshimiwa na jana nimetoa 150,” alijibu DPP Mganga kwa sauti ya chini

Advertisement

“Na jana umesema umetoa, njoo utoe sauti yako hapa wakusikie, ulitoa wangapi jana, ameuliza Rais akimtaka DPP Mganga kujibu

“Jana niliwafutia mahabusu 150 gereza la Geita” amesema DPP

“Kwa hiyo wamefika 751” amehoji Rais huku Mkurugenzi huyo wa Mashtaka akijibu “Ndio mheshimiwa”

 

Rais Magufuli alisema hao mahabusu waliosamehewa walipaswa kutolewa katika magereza siku nyingi

“Hao 150 maanake wamekaa mahabusu, wangetakiwa wawe wametolewa zamani, hao 601 wangetakiwa wawe wameshatoka kwenye mahabusu lakini wameshikwa wakawa wamesondekwa mule, saa nyingine wengine kwa kuonewa” amesema

“Kwa hiyo hakimu au jaji hawezi kujua kuna mahabusu wangapi kule kwa sababu yeye anategemea wale wanaopelekwa kwenye uamuzi, ndio maana kuwa na mahabusu wengi sio sababu ya mahakimu au majaji, sababu kubwa ni kwa hawa wengine ambao wanashindwa kutimiza wajibu wao” amesema

Amemuagiza DPP Mganga kutembelea magereza katika mikoa yote nchini ili kuwatoa mahabusu ambao hawastahili kukaa magerezani.

“Ndiyo maana nakupongeza Mganga, umekuwa mganga mzuri kwa mahabusu hawa, endelea utembelee katika mikoa yote, nchi hii sio ya kukaa mahabusu wakati wengine hawana makosa” amesema Rais Magufuli


Advertisement