Daktari adadavua upandikizaji mimba

Muktasari:

Ugumba unaelezwa kukumba wanandoa wengi nchini

Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imesema kuanzishwa kwa huduma ya upandikizaji mimba imetokana na idadi kubwa ya wanandoa wanaohitaji usaidizi wa kupata watoto, baada ya via vya uzazi kwa wanawake kuharibika huku wanaume wakiwa na mbegu zisizo na uwezo wa kusafiri haraka kulifikia yai lililorutubishwa.

Muhimbili imesema tatizo hilo linaongezeka kwa sasa kwani kitakwimu inahudumia wanawake wapatao 1,200 kwa mwaka, ambao wana tatizo la kutopata ujauzito na suluhu ni kuwapandikiza mimba.

Akizungumza na Mwananchi jana, daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi, Dk Vincent Tarimo alisema tatizo la mama kushindwa kupata mtoto lipo na linaongezeka kila siku huku akitaja chanzo ni hutokana na mirija yake kuwa na matatizo na inawezekana imeharibiwa na maambukizi kwenye mirija ya uzazi kwa kuharibiwa na wadudu.

“Kwa wastani mimi nikiwa kliniki huwa nahudumia mara moja kwa wiki kwa magonjwa yanayohusisha uzazi isipokuwa ujauzito, naona wagonjwa watano kwa siku wenye tatizo la ugumba,” alisema Dk Tarimo na kuongeza:

“Naweza kuona watano kwa hivyo kwa wastani kwa wiki Hospitali ya Muhimbili inaona wagonjwa si chini ya 25 na kwa mwezi tunaona wagonjwa 100, tunahesabu kwa mwaka ni 1,200.”

Alisema wanawake wanaweza kusaidiwa na kupandikizwa kwa kuruka njia ya asili tangu yai linapotoka kuweza kupita kwenye mirija mpaka kwenye mji wa mimba, kulivuna moja kwa moja likishakuwa tayari baada ya hapo anamsaidia kulipandikiza ndani ya kizazi chake hivyo, halipiti tena kwenye njia yake ya kawaida.

“Wenzetu walianza zamani, sisi tumechelewa kuanza lakini ni kitu kizuri ambacho kitawasaidia dada zetu, mama zetu na wadogo zetu ambao wanapata changamoto nyingi kwenye familia na ndoa zao wengine wanaachika sababu ya kushindwa kupata mimba,” alisema.

Hata hivyo, Dk Tarimo alisema tatizo hilo linachangiwa na pande mbili; mwanamke na mwanaume ingawa kwa Watanzania na Waafrika wengi lawama zinakwenda kwa mwanamke ambaye ndiye anabeba ujauzito.

“Unaweza kukuta huyu baba ana matatizo yanayomfanya ashidwe kupata mtoto kwa hiyo naye anaweza akasaidiwa kwa huduma kama uwezo wake ni mdogo. Kama shida anayo mwanamke peke yake ni mirija siyo mwanaume hiyo ni rahisi sana kufanyika,” alisema Dk Tarimo na kuongeza:

“Kwa kuwa utavuna yai la baba na mama kuna dawa utampa ya kustimulate (kuchochea) halafu unavuna yai la mama utaweka kwenye kifaa maalumu incubater halafu utampandikizia mama.”

Alisema ikiwa baba na mama kwa pamoja wana shida hasa baba idadi yake ya mbegu ni ndogo, tiba hiyo itatakiwa kuchagua yai lenye ubora au mbegu ndilo litakaloweza kutoa mtoto.

“Kuna idadi ya mbegu za baba inabidi uwe nayo ndiyo uweze kupata mtoto kuna zile zinazokwenda kwa kasi zifike mapema na kurutubisha yai la mama, kama hazipo zenye kasi au zipo chache basi kwa kutumia utaratibu huu unaweza kuchagua ambazo ni nzuri na ukazitumia kama baba unakuta mayai yake machache sana au mengi hayana kasi, kwa sababu mama huwa anatoa yai moja tu lakini baba huwa anatoa mengi kwa hiyo hapo unachagua linalofaa,” alisema.

Chanzo cha tatizo

Dk Tarimo alisema maisha yanachangia kwa kiwango kikubwa kuleta tatizo la ugumba kwa pande zote mbili.

“Wasichana wanaanza tendo la ndoa mapema kwa hivyo unakuta labda alianza tangu shule ya msingi, hivyo inamuongezea hatari ya kupata maambukizi katika via vya uzazi kwa hiyo unakuta ikiathiri mfumo wa uzazi inasababisha ugumba.

“Kuna wengine unakuta kwa sababu ni wadogo wanarubuniwa kutoa mimba sehemu ambayo si salama, anapata maambukizi ya hao wadudu kisha wanaharibu mfumo wa uzazi,” alisema.

Pia, alitaja sababu za wanaume kukumbwa na tatizo la ugumba. “Wengi kutokula vizuri, mwili hautumiki sana na tunakula vyakula ambavyo havina lishe na virutubisho kwa mtu kutoa mayai ambayo yana ubora, ulevi na mazingira ambayo joto ni kubwa, hivyo inaathiri uzalishaji wa mbegu na wengine wanatumia sigara, bangi vyote vinaathiri uzalishaji wa mbegu bora za kiume.”

Benki ya mbegu

Mtaalamu huyo alisema ni la kisheria linategemea uamuzi wa watunga sera na sheria kwa kuwa ni taratibu za nchi husika.

“Watu wa maadili wakae hata ikibidi viongozi wa kidini nao wakae hapo ndiyo kutakuwa na jibu sahihi, twende kwa namna gani maana kuna wengine mama hana kizazi kabisa lakini ana mayai,” alisema Dk Tarimo na kuongeza:

“Inawezekana likachukuliwa yai lake na la mume wake akapandikiziwa mama mwingine ambaye anakuwa anamtunzia tu mtoto lakini mtoto akizaliwa vinasaba vyote vinakuwa vya wanandoa husika, japokuwa hatujafika huko.”