Daktari bingwa aelezea maendeleo ya Askofu Mkuu Ruwa’ichi

Muktasari:

  • Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam nchini Tanzania, Muhashamu Yuda Thadaeus Ruwa’ichi anaendelea vyema na hivi karibuni anatarajiwa kuruhusiwa kutoka wodini katika Taasisi ya Mifupa (Moi), Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Maendeleo ya afya ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam nchini Tanzania, Muhashamu Yuda Thadaeus Ruwa’ichi yanawapa matumaini madaktari na huenda akaruhusiwa kutoka wodini hivi karibuni.

Septemba 10, 2019 Askofu Ruwa’ichi alifanyiwa upasuaji wa kuondoa damu kwenye ubongo katika Taasisi ya Mifupa (Moi) jijini Dar es Salaam anakoendelea kutibiwa hadi sasa.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Septemba 18,2019 Daktari bingwa wa upasuaji ubongo na mishipa ya fahamu Profesa Joseph Kahamba amesema kiongozi huyo wa kiroho atatoka hospitali hivi karibuni.

“Anaendelea vizuri mno, maendeleo yanatupa faraja hata sisi madaktari tunaomhudumia kila siku anaimarika na kuongeza kile alichofanya siku iliyopita.”

“Leo ametembea umbali mrefu tena mwenyewe kwenda na kurudi bila msaada wa mtu, anazungumza kama ninavyozungumza na wewe (akimaanisha mwandishi wa habari). Niwaambie tu mtamuona hivi karibuni,” amesema Profesa Kahamba

Hata hivyo, Profesa Kahamba amekataa kuelezea ni lini hasa askofu Ruwa’ichi ataruhusiwa kutoka hospitalini hapo.

Kwa sasa kiongozi huyo yupo katika wodi wa kawaida baada ya kuhamishiwa kutoka chumba cha uangalizi maalum (ICU) alikokaa kwa siku sita baada ya kufanyiwa upasuaji.