Dar yaongoza uandikishaji, Jiji la Arusha lanyooshewa kidole

Muktasari:

  • Wakati wadau wakieleza kusua sua kwa shughuli ya uandikishaji wapiga kura katika uchaguzi serikali za mitaa, Wazirichi Ofisi ya Rais Tamisemi Seleman Jafo amesifia kuwa shughuli inakwenda vizuri  na huenda wakavunja rekodi.
  • -Uandikishaji wapiga kura ulianza Oktoba 8 na utamalizika kesho Alhamisi Oktoba 17, 2019.

Dodoma. Mkoa wa Dar es Salaam umekuwa kinara katika uandikishaji wapiga kura wa uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019 baada ya kuandikisha asilimia 89 hadi leo Jumatano wakati mikoa ya Kigoma na Kilimanjaro ikivuta mkia kwa kuwa na asilimia ndogo.

Akitoa taarifa ya uandikishaji leo Jumatano Oktoba 16,2019, Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Seleman Jafo amesema baada ya kuongezwa kwa muda, shughuli imekwenda vizuri kwani mikoa yote imeandikisha juu ya asilimia 50.

Hata hivyo, Jafo amewanyooshea kidole watendaji katika Halmashauri ya Jiji la Arusha akiwataka kujitathimini kwani ni halmashauri pekee ambayo hadi leo uandikishaji wake uko chini ya asilimia 50 licha ya kuwa kimkoa Arusha ina asilimia 66.

"Hadi jana Oktoba 15, tulishaandikisha watu 16.9 milioni ambayo ni asilimia 74 hivyo zoezi linakwenda kwani wakuu wa mikoa na wilaya wameamua kufanya kazi na hivyo wanaelekea kuvunja rekodi kwa baadhi ya mikoa na halmashauri," amesema Jafo.

Waziri ametaja mikoa ambayo inaongoza na asilimia zao katika mabano ni Dar es Salaam (89), Pwani (86), Tanga (81), Mtwara (80) na mkoa wa Lindi uliofikisha asilimia 77 lakini mikoa ya chini ni Kigoma (57), Kilimanjaro (58), Arusha (66) na Shinyanga asilimia 66.