Dayosisi mbili zapinga wanawake KKKT kuwa wachungaji

Wanawake ambao ni wajumbe wa mkutano mkuu wa KKKT wakiwepo wachungaji wakiwa katika picha ya pamoja kuonesha mshikamano baada ya kuwepo baadhi ya Dayosisi ambazo hazitaki Wanawake kuwa wachungaji.
Picha Mussa Juma

Muktasari:

  • Mkutano Mkuu wa 20 wa Kanisa la Kiinjili  Kilutheri Tanzania (KKKT) unaendelea jijini Arusha ambapo pamoja na mijadala mbalimbali inayoendelea, wajumbe wa mkutano huo watamchagua Mkuu wa Kanisa hilo atakayeliongoza kwa kipindi cha miaka minne.

Arusha. Wajumbe wa mkutano Mkuu wa 20 kwa Kanisa la Kiinjili  Kilutheri Tanzania (KKKT) wamegawanyika kuhusiana na kuridhia wanawake kuteuliwa kuwa wachungaji.

Wajumbe hao kutoka katika Dayosisi 26 za Kanisa hilo, walipaswa kupitisha ajenda ya kuunga mkono wanawake kuteuliwa kuwa wachungaji katika Dayosisi zote kutokana na mchango wao katika Kanisa.

Hata hivyo, Dayosisi mbili, za Mbulu na Shinyanga walitajwa kuendelea na msimamo wa kuwapinga wanawake na Dayosisi ya Mara ikidaiwa kutokuwa na wachungaji wanawake wa kutosha.

Wakichangia hoja huyo katika mkutano huo leo Ijumaa Agosti 23,2019 baadhi ya wajumbe wameeleza tayari mkutano Mkuu wa Dodoma ulikwishapitisha jambo hilo lakini bado linapigwa.

Magdalena Mathayo ambaye ni muithologia kutoka Dayosisi ya Mbulu kitengo cha wanawake akizungumza na mwananchi nje ya ukumbi wa mkutano jijini Arusha amesema wanaopinga hoja hiyo ni waumini wachache ambao wanapaswa kuelimishwa.

Mathayo amesema wanawake hivi sasa wamesoma na wana uwezo wa kuendesha ibada ila kuna baadhi ya waumini wanapinga bila sababu.

"Pale Mbulu kwa sasa tupo wanawake wanne waetholojia ambao tunaweza kuwa wachungaji," amesema

Mkurugenzi wa idara ya wanawake na watoto Dayosisi ya Pare, Rosemary Solomon amesema jambo la wanawake kuwa wachungaji tayari lilipitishwa na alitaka hoja hiyo itekelezwe Dayosisi zote.

"Leo baada kuonekana bado kuna Dayosisi hazitaki wanawake kuwa wachungaji Askofu Mkuu ametoa maelekezo maaskofu wa Dayosisi nyingine kwenda kutoa elimu,” amesema

Amesema pia wajumbe wa halmashauri kuu wametakiwa kwenda kutoa elimu katika Dayosisi zinazopinga.

Askofu Steven Munga alitaka waumini wa kanisa hilo kutambua wao wote ni kitu kimoja hakuna sababu ya kutengana.

Mjumbe mwingine akizungumzia hoja hiyo, amesema hakubaliani na wanawake kuwa wachungaji kwani sio msingi wa kanisa.

Hata hivyo, baada ya mjadala Mkuu wa KKKT, Fredrick Shoo alipendekeza hoja hiyo itaendelea kujadiliwa ili kuongeza uelewa na mkutano ujao suala hilo limekwisha.

Imeandikwa na Mussa Juma, Zainabu Hassan na Elizabeth Elias.